Verified Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imetajwa kuwa ni miongoni mwa Hifadhi inayonufaika na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) ambapo kwa sasa ndege zaidi ya tisa za watalii zimekuwa zikitua kutokana na kukarabatiwa kwa kiwanja cha ndege cha Kikoboko hali iliyopelekea kuwepo kwa usalama wa kutosha kwa watalii.
Kufuatia maboresho hayo ya kiwanja cha ndege kumewezesha ndege kubwa zinazobeba abiria 42 kuweza kutua kwa urahisi tofauti na hapo awali ambapo ndege za abiria 12 pekee ndio zilizokuwa zinaweza kutua katika kiwanja hicho.
Mhifadhi Mkuu wa Idara ya Ujirani Mwema na Uhusiano, David Kadomo ametoa kauli hiyo leo April 27, 2023 wakati akielezea jinsi Mradi wa REGROW unavyoendelea kuleta mapinduzi makubwa katika Hifadhi hiyo iliyopo Mkoani Morogoro ambapo idadi ya watalii pia imeongeza kutoka watalii elfu 59 hadi watalii elfu 90.
Kutokana na uwekezaji wa mradi wa REGROW pamoja na filamu ya Royal Tour iliyotangaza vivutio vilivyopo nchini, Mhifadhi Kadomo amesema kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu Hifadhi hiyo inatarajia kupokea jumla ya watalii 100,000 na mapato Shilingi Bil.3.9 yatokanayo na watalii.
Mradi wa REGROW ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kwa kuendeleza Sekta ya Utalii katika Mikoa ya Kusini. Mradi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Milioni 150 kutoka Benki ya Dunia.