Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

REA kusambaza mitungi ya gesi vijijini

GESII WEBB REA kusambaza mitungi ya gesi vijijini

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Nishati Vijijini (REA), katika Mwaka huu wa Fedha (2023/24), umetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kusambaza mitungi ya gesi ya LPG, majiko na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini kwa njia ya ruzuku.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameyasema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Wakala kwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alipofanya kikao na Menejimenti ya Wakala huo Jijini Dodoma.

Alisema kuwa, kiasi cha mitungi kati ya 200,000 hadi 500,000 inatarajiwa kusambazwa katika maeneo ya vijijini kutegemea kiwango cha ruzuku kitakachotolewa.

Akielezea Mradi wa usambazaji gesi ya kupikia kwa ujumla, Mhandisi Saidy alisema unategemewa kusambaza mitungi ya gesi 70,020 ambapo hadi kufikia Agosti 15 mwaka huu, mitungi 23,806 (sawa na asilimia 34) ilikuwa imeshasambazwa kwa wananchi mbalimbali kupitia kwa Wabunge ambao ni wawakilishi wao.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa, katika hatua nyingine, REA inatekeleza Mradi wa usambazaji gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Lindi na Pwani kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo alisema Mkataba umesainiwa na maombi ya fedha za awali, yapo Wizara ya Fedha kwa ajili ya uhakiki.

“Mkataba huu una jumla ya shilingi bilioni 6.8 ambapo unatarajiwa kuunganisha wananchi 980 na nishati ya kupikia katika maeneo ya Mnazi Mmoja mkoani Lindi na Mkuranga mkoani Pwani.”

Mkurugenzi Mkuu pia alieleza kuhusu Mradi wa ufungaji mifumo ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300 ambapo alisema Wakala unalenga kujenga mifumo hiyo kwa Taasisi 100.

Akifafanua, alisema kuwa Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akifungua Kongamano la Nishati ya Kupikia jijini Dar es Salaam, Novemba 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live