Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Shigela anadi fursa za GGML zinazoipaisha Geita kongamano la madini

RC Shigela Anadi Fursa Za GGML Zinazoipaisha Geita Kongamano La Madini.jpeg RC Shigela anadi fursa za GGML zinazoipaisha Geita kongamano la madini

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania 2023 likifikia tamati tarehe 26 Oktoba mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela amebainisha fursa zinazotokana na uwepo wa kampuni kubwa ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuwa chanzo cha kupaisha mkoa huo kiuchumi.

Mbali na GGML, pia zipo kampuni za kati na wachimbaji wadogo ambao wametajwa kusisimua uchumi wa mkoa huo ambao unazalisha asilimia 60 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika kongamano hilo lililofungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Shigela amesema wamekuja kushiriki ili kuona mwelekeo wa sekta ya madini, teknolojia mpya inayotumika na namna wachimbaji wadogo wanavyowea kuitumia.

Amesema GGML ni miongoni mwa makampuni makubwa ambayo yanaongoza kwa kulipa kodi nchini lakini pia yanaongoza kwenye uzalishaji wa dhahabu.

Amesema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia sheria, sera, miongozo ambayo inamtaka waziri wa madini kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki katika uchimbaji kwa kupewa leseni za umiliki, zimezidi kuipaisha sekta hiyo.

Ametoa mfano kuwa karibu asilimia 30 ya ya dhababu inayozalishwa mkoani Geita inatoka kwa wachimbaji wadogo huku asilimia 70 ikitoka kwa wachimbaji wakubwa.

“Maana yake ni kwamba rasilimali ya madini iliyopo katika mkoa wetu wa Geita inawafaidisha watanzania wote ikiwamo wenye mtaji na wasio na mtaji ambao pia wanataka kuingia kwenye sekta ya madini na mkoa pekee ambao wanaweza kuchimba kwa uhakika ni Geita.

Ameongeza katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia wamezalisha dhahabu zaidi ya tani 47 zenye thamani ya Sh trilioni sita na katika hizo tani 11 zinatokana na wachimbaji wadogo na 36 ni kwa wachimbaji wakubwa.

Aidha, amesema uzoefu ambao wameupata kwenye sekta ya madini, ni pamoja na kupata fedha za kigeni kwa sababu ya kuuza dhahabu,

“Kwenye suala la ajira, mathalani kwa GGML peke yake imetengeneza ajira kwa watanzania zaidi ya 6000.

“Wananchi wanafanya biashara, manunuzi peke yake ya GGML kwa mwaka yanafikia zaidi ya Sh trilioni moja. Wananunua chakula, mavazi kwa ajili ya shughuli za uchimbaji, wananunua mafuta, wanatumia magari kusafirisha bidhaa, wanatumia malori na mabasi kusafirisha wafanyakazi zote hizi ni huduma ambazo zinapatikana Geita kupitia GGML,” amesema na kuongeza;

“Lakini wapo wafanyabiashara ambao wanafanya biashara za hoteli wapo wafanyakazi ambao wanakuja kwenye mgodi, wapo wafanyabiashara wanakuja kununua dhahabu,” amesema.

Ameongeza mbali na Geita kuwa na soko la dhahabu, pia eneo la tatu ni faida itokanayo na mahusiano kati ya migodi na wananchi ambapo mkoa huo unafaidika na mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kutoka GGML peke yake wenye thamani ya Sh bilioni tisa kila mwaka.

Amesisitiza Halmashauri ya Mji wa Geita na wilaya ya Geita hupanga bajeti ili fedha hizo zirudishe huduma kwa jamii ikiwamo kugusa sekta ya maji, elimu, afya na sekta za uzalishaji.

Katika uzalishaji alitoa mfano shughuli za kilimo pamoja na wafanyabiashara ndogondogo ambao wanawezeshwa na GGML kupitia jitihada hizo za uzalishaji na kukuza sekta ya madini.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa wanazozipata kutokaja na uwepo wa rasilimali hizo kwa kuweka akiba na kufungua biashara mbalimbali.

Pia aliwataka wamiliki wa migodi ambao hawajanza kutekeleza mpango huo wa CSR kushirikiana na jamii inayowazunguka lakini pia kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live