Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Mbeya aagiza maofisa biashara kujitathimi

Rc Mbeya Pic Data RC Mbeya aagiza maofisa biashara kujitathimi

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Juma Homera amewataka maofisa biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kujitathimi utendaji wa kazi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao na kupelekea wawekezaji kuondoka na kwenda maeneo mengine.

Homera ametoa agizo hilo leo Jumanne Machi 15, 2022 kwenye kikao kazi cha maofisa biashara kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa kilichoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na kufanyika jijini Mbeya.

Homera amesema kuwa Serikali ina malengo makubwa ya kuvutua wawekezaji lakini kuna tatizo la baadhi ya maofisa biashara kukaa ofisini badala ya kubuni namna ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo hayo hivyo kuwafanya wawekezaji kuondoka na kupelekea kuikosesha   Serikali mapato.

''Leo baada ya kikao hiki nitawasiliana na wakuu wa mikoa wenzangu kuanza ufuatiliaji na ifikapo mwezi June mwakani tutahitaji mlete mrejesho wa mpango kazi unaonyesha idadi ya wawekezaji waliongezeka na leseni zilizotolewa hicho kitakuwa kipimo chenu kama mnafaa au la ''amesema.

Amesema umefika wakati kila mmoja ajipime utendaji wake wa kazi kwani lengo ni kuondoa watendaji ambao ni mizigo.

'''Kuna  mwekezaji  mkubwa alikuja kwa ajili ya kuwekeza kiwanda cha nondo na uchimbaji wa madini lakini amekwama na kuondoka shida ni vitu vidogovidogo  ambavyo havina msingi sasa tunapoteza mapato kwa sababu ya maofisa biashara wasiojua majukumu yao ''amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa amesema kuwa wamebaini baadhi ya maofisa biashara katika halmashauri wamekuwa wakitoa kiholela leseni daraja kwa gharama nafuu jambo linalosababishia Serikali kupata hasara.

''Tumebaini hilo kwani leseni daraja (A) zinapaswa kutolewa na Brela na sio halmashauri ninawasihi maofisa biashara kufanya kazi kwa weledi na kubadilika katika utendaji wa kazi'' amesema.

Ofisa biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Denis Mzimilu amesema wataendelea kushirikiana na halmashauri nchini kuona namna bora ya kuwawezesha maofisa biashara kutekeleza majukumu yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live