Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla amesema Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ina uwezo mkubwa wa kubeba bidhaa mbalimbali kwa kutumia ndege yake mpya ya kisasa ya mizigo aina ya Boeing 767-300F.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja cha wadau wa soko la bidhaa za samaki kutoka mkoani Mwanza kilichofanyika ATCL Makao Makuu, Dar es Salaam, Makalla amesema kuwepo kwa ndege hiyo kunarahisisha usafirishaji wa bidhaa za kitanzania hususani minofu ya samaki kwa kuweza kusafirishwa moja kwa moja kutoka kanda ya ziwa kwenda kwenye masoko mbalimbali duniani.
Amefafanua kuwa Ndege hiyo inawawezesha wafanyabiashara wa minofu ya samaki kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza thamani ya minofu kwa kutumia muda mfupi kufika kwenye soko la walaji.
Aidha, Makalla amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa wataendelea kushirikisha wadau na wataalam mbalimbali katika kushughulikia changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya uwanja wa ndege wa Mwanza hususan jengo la kuhifadhia bidhaa, uwepo wa kituo kimoja cha utoaji wa huduma za mamlaka zote za uthibiti, kupitia tozo na taratibu ili kupunguza gharama zisizo za lazima na kuhakikisha bidhaa hizo zinasafirishwa kupitia kiwanja cha ndege cha Mwanza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mha. Ladislaus Matindi amesema Air Tanzania pamoja na kufanyabiashara inahusika pia na uwezeshaji wa sekta zingine kwa kutoa huduma zinazohitajika ikiwemo kulinda thamani ya bidhaa za Watanzania kwa kuzifikisha kwenye soko la dunia zikiwa shindani.
Matindi ameongeza kuwa uwepo wa Ndege ya mizigo yenye uwezo wa kubeba mizigo yenye upana mkubwa na uzito wa zaidi tani 50 kwa mara moja ni fursa kwa Watanzania kukuza biashara zao duniani.