Dodoma. Katika jitihada za kurahisisha usafiri, Shirika la Ndege la Precision limezindua safari kutoka Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma leo.
Licha ya safari hizo, shirika hilo pia litakuwa linasafari za kutoka Dodoma kwenda Kilimanjaro.
Akizungumzia uzinduzi wa safari hizo leo, Jumatatu ya Aprili Mosi, kaimu mkurugenzi wa Precision Air, Patrick Mwanri amesema ni furaha kubwa kwao kuchangia juhudi za Serikali kuendeleza na kuyafungua makao makuu ya nchi kwa usafiri wa anga.
“Kwa miaka 25 tumekuwa tukiiunganisha Tanzania na kuhakikisha abiria wanasafiri kwa urahisi ndani na nje ya nchi. Safari zetu za Dodoma zitarahisisha shughuli za utawala na biashara kati ya Dodoma na mikoa mengine,” amesema.
Katika kuhakikisha huduma zao zinakuwa rafiki kwa abiria waliopo, Mwanri amesema watakuwa na uhuru wa kuchagua muda wa kusafiri kwani ndege zitakuwa zikiondoka saa 1:00 asubuhi, saa 3:25 asubuhi na saa 7:50 mchana kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na saa 2:25 asubuhi, saa 4:55 asubuhi na saa 10:55 jioni kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Shirika hilo litakuwa linafanya safari zake kwa siku sita kila wiki na Mwanri amefafanua kuwa ndege zitakuwa zinatoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kila Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Jumamosi huku Alhamisi na Ijumaa zikipitia Kilimanjaro.
Akizungumzia uzinduzi wa safari hizo mkuu wa wilaya ya Dodoma aliyemwakilisha mkuu wa mkoa, Patrobas Katambi amelitaka Precision kuongeza safari kati ya Dodoma na mikoa mingine ili kuhamasisha na kuchangamsha zaidi uchumi.
“ATCL wapo na wanasafiri kati ya Dodoma na Dar es Salaam. ninyi nawaomba muongeze safari kwenda mikoa mingine kama Kigoma na Mwanza. Tunapokea wageni wengi hapa ambao wakimaliza kuongea na viongozi angependa kutembelea Gombe (Kigoma) au Mwanza lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa kuwa hakuna usafiri,” amesema Katambi.
Tangu lilipoanzishwa mwaka 1993, shirika la Precision linafanya safari zake kutokea Dar es Salaam kuelekea Arusha, Bukoba, Kilimanjaro, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kahama na Zanzibar. Vilevile linatua Nairobi, Kenya na Entebbe, Uganda.
Mmoja wa abiria wa usafiri huo, Athile Mputa amesema Precision itasaidia kuimarisha huduma kwani mwanzo hakukuwa na mbadala wa kutosha.
“Ukiikosa ATCL ulilazimika kutumia barabara au ukodi ndege. Kwa wananchi wenye kipato cha kawaida huwezi kukodi ndege hivyo unalazimika kutumia barabara. Changamoto ya huko ni kutumia muda mwingi,” amesema Mputa.