Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Posta watakiwa kujiendesha kisasa kwa faida

9c8fd8cebe95f752253482db3adc00f6 Posta watakiwa kujiendesha kisasa kwa faida

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulie ameliagiza Shirika la Posta Tanzania kujiendesha kisasa na hataki kusikia habari za kujiendesha kihasara.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa 27 wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, Dk Ndugulile alisema Shirika la la Posta lina rasilimali nyingi ambazo wanaweza kuzitumia kama fursa ya kujiendesha.

"Shirika lina rasilimali nyingi, hili shirika ni tajiri wa rasilimali ambazo mnaweze kuzitumia katika kuongezea shirika mapato, hivyo sitarajii kusikia shirika linajiendesha kihasara. Tumieni rasilimali kwa ustawi wa shirika na si ustawi wa mtu binafsi,

"Jiendesheni mzalishe na kupata mapato, msitarajie mimi kwenda kwa Rais (John Magufuli) kuomba fedha za ninyi kuongezewa mishahara hilo sitalifanya, Rais ni mtu wa mahesabu na anayehitaji matokeo, atataka kuona fedha zinazoombwa na kuzitoa zitaleta matokeo gani,"alisema.

Aidha, Dk Ndugulile amemtaka Postamasta Mkuu, Hassan Mwang'ombe kuhakikisha anaimarisha kitengo cha utafiti, ubunifu na masoko ili kuja na bidhaa nyingi zinatakazoliingizia shirika mapato.

"Mimi niwaahidi kuwa nitawapa ushirikiano mkubwa, lakini ninataka matokeo chanya. Pia niwapongeze kwa hatua mliyoianza ya kuja na Posta kiganjani,

"Changamoto kubwa mliyonayo ni ushindani mkubwa uliopo na teknolojia ya dijitali, lakini hii mnaiweza kutumia kuwa fursa kwa kuja na bidhaa zingine, hivyo imarisheni kitengo cha utafiri, ubunifu na masoko".

Alitaka maazimio watakayofikia hapo wayapeleke kwake na yawe maazimio yanayopimika na hayo ndiyo yatakayokuwa mkataba kati yake na wao.

Pia alikemea tabia ya watumishi hususani ofisi za mikoa ambazo zimekuwa zikichelewa hata kufungua ofisi.

"Mimi ninapata taarifa zenu kila mahali sasa mbadilike, hii tabia ya kuchelewa kufungua ofisi na mkifika ofisini mwende kunywa chai iiachwe kabisa, atakayendelea nayo basi tutamng'oa huko huko,"alisema.

Pia Dk Ndugulile alisisitiza haja ya shirika hilo kufanya maboresho ya Sera ya Posta, sheria ili iendane na mahitaji ya sasa na pia kupitia muundo wa shirika ili uendana na hali ya sasa na uwe muundo unaorahisisha usimamizi na utendaji wa shirika.

Naye Postamasta Mkuu, Mwang'ombe alisema kikao hicho kitakuwa na kazi kujadili maendeleo ya shirika, mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa mwaka mmoja, sheria ya utumishi wa umma, wajibu na maslahi yao, nidhamu na mahusiano mahali pa kazi.

Chanzo: habarileo.co.tz