Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yataka wamiliki wa malori kuwasimamia madereva wao

MALORI 1 780x470 Polisi yataka wamiliki wa malori kuwasimamia madereva wao

Wed, 20 Dec 2023 Chanzo: mwanachidigital

eshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limewataka wamiliki wa malori kuwasimamia kwa karibu madereva wao ili kuepusha ajali.

Usimamizi pia umeelezwa utawaepusha na matukio ya uhalifu wawapo safarini, kama vile kubeba wahamiaji haramu.

Mkuu wa dawati la usalama barabarani, Michael Steven amesema hayo jana Desemba 19,2023 katika mkutano mkuu wa nne wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya kati na madogo (Tamstoa).

New Content Item (1)

Steven amesema mara kwa mara madereva wamekuwa wakisababisha ajali ambazo kwa kiasi kikubwa chanzo ni uzembe wao wawapo barabarani.

Kuhusu uhalifu amesema baadhi wamekuwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi na wahamiaji haramu kwenye makontena na matangi yanayobebea mafuta.

“Ni vyema mkawadhibiti madereva hawa tangu mnapowapa ajira ili sekta hii iwe salama katika kipindi chote, kwani wapo wanaodiriki kusababisha ajali kwa kukusudia wakiangusha matanki ili waibe mafuta, lakini unapoenda kuangalia mafuta yaliyomwagika na uhalisia wa ajali ni tofauti,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani amesema wataendelea kutoa elimu kwa madereva mara kwa mara na watakaoonekana wameshindikana hawatasita kuwachukulia hatua.

Shabani amesema endapo dereva atabainika kuwa na makosa yanayomuhusu mwenyewe ni vyema akabeba matatizo yake badala ya kumuhusisha mmiliki kwa kutaifisha gari lake.

Amesema wamepeleka mapendekezo ya kubadilishwa sheria bungeni kuhusu suala hilo.

“Si sahihi dereva kabeba bangi huko, wahamiaji haramu, halafu anakuja kuadhibiwa mmiliki ambaye wakati huo amelala nyumbani kwa kutaifishiwa chombo chake,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa chama cha madereva wa masafa marefu, Hassan Dede amesema hayo yote yanafanyika kutokana na masilahi duni kwa madereva.

Dede amesema mshahara wa Sh350,000 wanaolipwa madereva kwa mwezi hautoshelezi mahitaji yao na familia, hivyo wengine kujikuta wakishawishika kujihusisha na uhalifu.

“Leo Rais Samia Suluhu Hassan anafungua uchumi wetu kwa kuboresha na kuitanua bandari, lakini kama hatutajipanga kuwa na madereva wazuri, ikiwamo kuwalipa masilahi bora hatutaweza kuboresha uchumi wa nchi zaidi ya kutengeneza madereva wezi kutokana na ubinafsi wa wamiliki wa kujifikiria wao kupata faida na kutowathamini wanaowafanyia kazi,” amesema Dede.

Hata hivyo, amewapongeza Tamstoa kwamba wamekuwa wakijitahidi kujali masilahi ya madereva wao, kwani wakati kima cha chini cha Serikali kikiwa Sh350,000 wao wanalipa kuanzia Sh500,000.

Amewataka wamiliki wengine kuboresha mishahara.

Kuhusu mkutano

Akizungumzia mkutano huo, Shabani amesema unalenga kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji, changamoto na mafanikio waliyoyapata.

Amesema wameshughulikia migogoro mbalimbali ya sekta ya usafirishaji kwa kushirikina na Serikali, ukiwamo wa hivi karibuni wa kushikiliwa malori zaidi ya 250 kwa siku 40 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC).

Pia mgomo wa madereva wakidai haki ya kupewa fedha za dharura.

Kuhusu changamoto, amesema wanakabiliwa na matukio ya kutekwa kwa madereva na mali katika nchi ambazo wanasafirisha mizigo.

Amesema wameunda kamati ya utatu ili kushughulikia suala hilo, ambapo Tamstoa ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo.

Shabani amesema changamoto nyingine ni ufinyu wa barabara maeneo ya Tunduma na kukosekana maegesho ya magari kuanzia Dar es Salam hadi Tunduma, hivyo kulazimika kusimama kwenye vituo vya mabasi au stendi za mabasi ambako wakikutwa wanatozwa faini na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara katika ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Msadizi Huduma za Barabara, Andrew Magombana amesema watakutana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) na Tanroads kutatua changamoto hizo kwa wakati.

Magombana amesema Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wasafirishaji kuhakikisha inaweka mazingira rafiki ya kufanyia biashara zao.

Chanzo: mwanachidigital