Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pinda ataka mboga ziinufaishe Afrika

4fd4ebcc421375365d8809b38f2cf8ae Pinda ataka mboga ziinufaishe Afrika

Wed, 27 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema Afrika ina zaidi ya aina 400 za mazao ya mboga za asili, lakini ni chache tu zinatumika kwa chakula na biashara.

Akizungumza mjini Arusha juzi, Pinda alisema jitihada za ziada zinahitajika kuhakikisha aina hizo zote za mboga zinatumika kwa chakula na biashara kwa faida ya nchi na bara la Afrika.

Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa taasisi za kilimo nchini na nje ya nchi, wadau na watafiti wa mboga wa ndani na nje ya nchi.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wafanyabiashara wa mboga kwa lengo la kuboresha zaidi kilimo cha mazao hayo ili yatumike kwa biashara na chakula.

Mkutano huo uliandaliwa na Kituo cha World vegetable cha jijini Arusha.

Pinda alisema mboga za asili barani Afrika ni urithi wa Waafrika hivyo mazao hayo lazima yatunzwe na kuenziwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kuitunza bioanuai isipotee.

Alisema utafiti unaonyesha kuwa, kutokana na kutofanyiwa utafiti wa kutosha na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, mimea ya mboga hasa ambayo hazilimwi inazidi kupotea kwa kasi na kusababisha hasara kwa Afrika na dunia.

Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema mazao ya mboga za asili ni muhimu kwa afya na lishe na kwamba utafiti wa kitaalamu unaonesha zina viwango vikubwa vya viini lishe ikilinganishwa na mboga nyingine kutoka mataifa ya nje ya bara la Afrika.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kuna takribani watu milioni 821 wanaokabiliwa na matatizo ya utapiamlo yanayotokana na kula chakula kisichokuwa na viini lishe bora.

Alisema kwa Tanzania, takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa watoto wenye umri wa miaka 0-5 wapatao milioni 3 wamedumaa, watoto wenye umri wa miaka 0-5 wapatao milioni 1.3 wana uzito pungufu na watoto wa umri wa miaka 0-5 wapatao milioni 5 wana upungufu wa damu.

Aidha, alisema watoto wenye umri wa miaka miaka 0-5 wapatao milioni 3 wana upungufu wa vitamini A na asilimia 32 ya wanawake wenye umri wa miaka miaka 14 – 49 wana tatizo la uzito uliozidi.

Pinda alisema serikali kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo imeamua kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025 kuweka uzito mkubwa kwa kuahidi kufanyia kazi changamoto hizo na ikibidi kuzimaliza.

Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Taasisi ya World Vegetable Centre, Dk Gabriel Rugalema alisema lengo la mkutano huo mbali ya kuhamashisha wakulima nchini kulima mboga, ni kutaka zao la mboga kuwa zao kuu la biashara ili liweze kuingizia nchi mapato

Chanzo: habarileo.co.tz