Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Petroli yashuka bei

F22b67c47a3a01ebbdce89d6ae73b726 Petroli yashuka bei

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ambazo zimeshuka ikiwemo petroli iliyoshuka kwa Sh 37.

Taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, ilisema mabadiliko hayo ya bei yamechangiwa na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Chibulunje alisema bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Novemba 4, mwaka huu.

Alisema kwa mwezi huu, bei za rejareja za petroli imepungua kwa Sh 37 kwa lita sawa na asilimia 1.97, dizeli Sh 47 kwa lita sawa na asilimia 2.71 na mafuta ya taa Sh 86 kwa lita sawa na asilimia 5.05.

Mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zilipungua kwa Sh 37.36 kwa lita sawa na asilimia 2.11, Sh 46.81 kwa lita sawa na asilimia 2.92 na Sh 86.02 kwa lita sawa na asilimia 5.44.

Chibulunje alisema kwa mikoa ya Kaskazini ukiwemo Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mwezi huu zimebadilika ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Alisema katika mikoa hiyo bei za rejareja za petroli na dizeli zimepungua kwa Sh 107 kwa lita sawa na asilimia 5.60 na Sh 27 kwa lita sawa na asilimia 1.59 ikilinganishwa na mwezi uliopita ambapo bei ya jumla ya petroli na dizeli ilipungua kwa Sh 106.40 kwa lita sawa na asilimia 5.99 na Sh 27.28 kwa lita sawa na asilimia 1.71 mtawalia.

“Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Novemba 4, mwaka huu, hii ni kwa sababu kwa mwezi Novemba mwaka huu, hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” alisema Chibulunje.

Kwa mujibu wa Chibulunje, mikoa ya Kusini ukiwemo Mtwara, Lindi na Ruvuma, bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli kwa mwezi huu zimebadilika ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Alisema kwa mwezi huu bei za rejareja za petroli na dizeli zimepungua kwa Sh 70 kwa lita sawa na asilimia 3.65 na Sh nne kwa lita sawa na asilimia 0.25 mtawalia ikilinganishwa na mwezi uliopita ambapo bei za jumla za petroli na dizeli zilipungua kwa Sh 69.38 kwa lita sawa na asilimia 3.91 na Sh 4.32 kwa lita sawa na asilimia 0.27 mtawalia.

Kutokana na mabadiliko hayo ya bei, Ewura imevita vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika kwa kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja.

Chanzo: habarileo.co.tz