Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Petroli, mkaa vyaongeza mfumuko wa bei

Mkaa Dar Matumizi Petroli, mkaa vyaongeza mfumuko wa bei

Fri, 10 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MFUMUKO wa bei wa taifa kwa Aprili 2024 umeongezeka kutoka asilimia tatu Machi, mwaka huu hadi asilimia 3.1.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu (NBS), Dk Albina Chuwa inaonesha ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula.

“Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa Aprili 2024 ikilinganishwa na Machi 2024 ni mkaa ambao mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 15.7 hadi 21.5,” alisema.

Pia samani za nyumbani mfumuko umepanda kutoka asilimia 4.5 hadi 4.8, magodoro kutoka asilimia 3.5 hadi 5.1, huduma ya malazi kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni kutoka asilimia 2.6 hadi 3.8, petroli bei imeongezeka kwa asilimia 2.1 na mafuta ya taa bei imeongezeka kwa asilimia hadi mbili.

Dk Chuwa alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Aprili, mwaka huu, umebaki katika asilimia 1.4 kama ilivyokuwa kwa Machi, mwaka huu. Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi ulioishia Aprili mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 3.7 kwa Machi, mwaka huu.

Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula visivyochakatwa, nishati na ankara za maji kwa Aprili, mwaka huu, umebaki katika asilimia 3.9 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Machi, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live