Serikali ya Zanzibar mwaka ujao wa fedha 2022/2023 imejipanga kuhakikisha maeneo huru ya biashara Micheweni, kisiwani Pemba yanaendelezwa kwa kuwekwa miundombinu ya barabara kwa ajili ya kukifungua kisiwa hicho kiuchumi na uwekezaji.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uwezeshaji na Uchumi, Mudrik Ramadhan Soraga wakati akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotaka kujua mikakati ya serikali kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuwekezaji.
Alitaja mikakati hiyo ni kukifungua Kisiwa cha Pemba katika miundombinu yake ikiwamo ya barabara na kusambaza nishati ya umeme hadi vijijini.
Alisema mikakati ya Serikali ya Zanzibar ni kukifanya Kisiwa cha Pemba kiwe cha uwekezaji na lango kuu la biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki.
Aliitaja mikakati mingine ni kujenga Kiwanja cha Ndege cha Pemba ili kufungua milango ya uwekezaji kwa wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali sambamba na utalii.
“Mipango inakwenda vizuri ambapo serikali ipo katika hatua za kutafuta wafadhili watakaosaidia ujenzi wa kiwanja cha ndege na tayari kazi za kulipa fidia kwa watu walioathirika na vitu vyao ikiwamo kuvunjiwa nyumba kupisha ujenzi huo zinaendelea.”
Aidha, alisema Serikali ya Zanzibar inaendelea na juhudi za kutafuta fedha za mkopo wa Euro milioni 460 kupitia mfuko wa kuhamasisha biashara kutoka Uingereza kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara za vijijini zenye urefu wa kilometa 103.5.
Akitoa ufafanuzi wa ziada, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Ali Suleiman Ameir alisema katika kuimarisha miundombinu ya barabara za vijijini, serikali inakusudia kujenga Barabara ya Chake Chake hadi Wete yenye urefu wa kilometa 21.2 ambayo itaunganisha mikoa miwili ya Kisiwa cha Pemba.
Alisema maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo yamekamilika na serikali ipo katika mchakato wa kutafuta mkandarasi atakayefanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa.
Aidha, alizitaja bandari tatu katika Kisiwa cha Pemba zitajengwa na moja kufanyiwa matengenezo makubwa ikiwamo ya Mkoani kwa ajili ya kuunganisha nchi za Afrika Mashariki kwa kutoa huduma kwa haraka.
Alizitaja bandari nyingine ambazo zitafanyiwa matengenezo makubwa ni Shumba Mjini na Wete kwa ajili ya kutoa huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria.
''Hiyo ndiyo mikakati itakayotekelezwa katika ujenzi wa miundombinu ya Kisiwa cha Pemba kukifanya kuwa lango kuu la uwekezaji wa miradi pamoja na kukitangaza kiutalii,'' alisema.