Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pato la Taifa lazidi kupaa

22a12dac9fca34cd02b8e6d6c6e62794 Pato la taifa laongezeka

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema Pato la Taifa katika robo ya kwanza ya Januari hadi Machi mwaka huu limeongezeka hadi Sh trilioni 38.0 kutoka Sh trilioni 36.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa alisema jana Dodoma kuwa, Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2015 limeongezeka hadi Sh trioni 33.2 katika robo ya kwanza ya mwaka huu kutoka Sh trioni 31.7 katika kipindi kama hicho mwaka jana sawa na ukuaji kwa asilimia 4.9.

Masolwa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, shughuli za uchimbaji wa madini na mawe umeongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha ukuaji kwa asilimia 10.2.

Alisema uchimbaji ulifuatiwa na habari na mawasiliano asilimia 9.1, uchukuzi na uhifadhi mizigo asilimia 9, maji na majitaka asilimia 9, huduma za kitaalamu, sayansi na ufundi asilimia 7.8, huduma zinazohusiana na utawala asilimia 7.4 na umeme asilimia 7.2

Katika mchango wa shughuli kuu za kiuchumi, Masolwa alisema, huduma zilichangia asilimia 40.1 ya Pato la Taifa ikifuatiwa na shughuli za msingi asilimia 37.1 na shughuli za kati asilimia 22.7.

Alisema ukuaji wa Pato la Taifa katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa asilimia 4.9 umechangia na shughuli zote za kiuchumi zilizofanyika nchini katika kipindi hicho.

Masolwa alisema mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa ulitokana na shughuli za kiuchumi za ujenzi kwa asilimia 14.9, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo kwa asilimia 14.6, kilimo kwa asilimia 12.7, uzalishaji viwanda kwa asilimia 9.8 na uchimbaji wa madini na mawe kwa asilimia 8.8.

Alisema ukokotoaji wa Pato la Taifa umezingatia matakwa ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kutayarisha takwimu za pato hilo unaojulikana kama System of National Accounts 2008 kwa lengo la kutayarisha takwimu linganifu kati ya nchi moja na nyingine.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351, takwimu hizi za Pato la Taifa kwa robo ya kwanza kwa mwaka huu ni rasmi na zinatumika katika kufuatilia na kutathmini malengo yaliyowekwa katika sekta za kiuchumi,” alisema Masolwa.

Alisema uwapo wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (covid-19) kwa kiasi kikubwa uliathiri utalii nchini.

"Tuendelee kuimarisha sekta nyingine ambazo haziusiani na utalii, sekta zinazotegemea utalii zimeathirika kwa kiwango kikubwa sana," alisema na kutaja sekta nyingine zilizoathirika kuwa ni hoteli na huduma za vyakula.

Chanzo: www.habarileo.co.tz