Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pass kuajiri vijana 700,000 katika kilimo

53130 VIJANA+PIC

Fri, 19 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika uwezeshaji wa kilimo (Pass) limejipanga kudhamini mikopo ya thamani Sh210.6 bilioni itakayoajiri watu 700,000 katika kilimo kuanzia 2019 hadi 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Aprili 18,2019 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa shirika hilo, Nicomed Bohay amesema mikopo hiyo itazinufaisha familia 235,253.

"Watu tunaowahudumia ni wajasiriamali wa biashara za kilimo, vyama na vikundi vya wakulima wadogo na kampuni zinazojihusisha na kilimo," amesema Bohay.

Katika mkakati huo, Bohay amesema wameanzisha kituo cha ubunifu wa kilimo (AIC) kilichopo mkoani Morogoro ambacho hutoa mafunzo ya kilimo cha biashara.

"Pia, tunaangalia fursa kwa vijana, kuna vijana 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tumeanzisha matumizi ya vijana ili kuwasaidia kuingia kwenye sekta ya kilimo," amesema.

Akizungumzia mafanikio ya shirika hilo kwa miaka 18, Bohay amesema wameshanufaisha wajasiriamali wa kilimo 929,172 waliopewa mikopo ya Sh712 bilioni na benki kwa udhamini wao.

"Mwaka 2018, Pass ilinufaisha biashara 196,873 zinazohusisha mazao na huduma kwenye kilimo," amesema.

Amezitaja benki wanazoshirikiana nazo kuwa ni CRDB, NMB, Benki ya Uwekezaji (TIB), ABC, Akiba Commercial Bank, Bank of Africa, Amanda Bank, Equity, Mkombozi, Access, Benki ya Posts, Vision Fund Microfinance, Azania, NBC na Benki ya Maendeleo ya Kilimo.



Chanzo: mwananchi.co.tz