Taasisi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo iitwayo Pass Trust imeanzisha Kampuni tanzu iitwayo PASS LEASING ili kupanua wigo wa huduma zake ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa asilimia 80 ya zana za kilimo na Viwanda bila dhamana kwa kushirikiana na Wasambazaji wa zana hizo.
Mkurugenzi wa Masoko wa PASS Adam Kamanda ametoa taarifa hiyo kwenye mkutano wa mashauriano na Wadau wa sekta ya kilimo wa kuhamasisha uzalishaji unaozingatia ukuaji wa kijani shirikishi uliofanyika Mkoani Tabora ambapo Kamanda akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PASS Yohana Kaduma, alisema kwa miaka 23 iliyopita PASS imewanufaisha Wajasiriamali milioni 3.4 Tanzania na kutoa ajira milioni 2.7 huku kati yao asilimia 51 wakiwa ni Wanawake na wameshirikiana na Benki 14 kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.3.
Mkutano huu ulikwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Kijanisha maisha na programu ya ukuaji wa kijani katika maisha kwa Kanda ya Kaskazini na Magharibi ambapo akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliipongeza PASS kwa kuja na mpango wa kukuza uchumi kupitia ajenda ya ukuaji shirikishi kama njia bora ya kuchochea kilimo endelevu huku Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ezekiel Mwansasu akizitaka Taasisi za fedha kuwa karibu zaidi na PASS ili kuwakomboa Watanzania.