Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Palestina yajitokeza kuunga mkono Tanzania ya Viwanda

24078 PALESTINA+PIC TanzaniaWeb

Sat, 27 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Balozi wa Palestina nchini, Hamdi Mansour Abuali amesema amekuwa kwenye majadiliano na Serikali ya jinsi ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 25, 2018 jijini Dar es Salaam, Balozi Abuali ametaja sekta mbili za kilimo na afya akisema wataanza nayo katika uchumi wa viwanda.

“Eneo mojawapo ni kwenye kilimo ambapo tumebadili mazao yetu kwa kusindika na kuuza nchi mbalimbali ikiwemo Israel. Nyingine ni Marekani, Ulaya wananunua na nchi za Kiarabu pia,” alisema Balozi Abuali.

“Tunakusudia kilimo cha kipekee kitakachofanyika hata kwenye maeneo yenye ukame kwa lengo la kuboresha. Kwa bahati nzuri Tanzania mnazalisha mazao mengi lakini hayachakatwi bali ni ya kutumia hapa hapa.”

“Tunataka kufanya usindikaji wa mazao kwa ajili ya kutumika kwa njia mbalimbali na kuuza nje ya nchi,” ameongeza. 

Amesema nchi hiyo inataka kuleta uzoefu wa kilimo unaotumia eneo dogo la ardhi lakini unakuwa na uzalishaji mkubwa na kufanya usindikaji wa mazao ya kilimo kibiashara.

“Uzoefu huo tumeupeleka katika nchi kadhaa kama Amerika Kusini, Afrika Kusini na hata nchi za Asia. Tungependa kumshirikisha Rais Magufuli kuibadilisha nchi hii iwe ya viwanda. Tunao utaalamu na teknolojia inayoweza kusaidia. Tunayo malengo yanayoweza kuleta bidhaa bora,” amesema.

Pamoja na mazao ya mimea, Balozi Abuali amesema wanazo teknolojia za kusindika mazao ya wanyama utaalamu wa kutumia ardhi ndogo kuzalisha mazao mengi.

Kuhusu sekta ya afya amesema Palestina inataka kufufua ushirikiano uliolala kwa muda mrefu kwa kusaini makubaliano na Wizara ya Afya ili kuisaidia Serikali.

“Kwa sasa tuko kwenye hatua ya kutia saini makubaliano na kuainisha maeneo ya ushirikiano na hapo ndipo tulipo. Kila upande unajipanga kuangalia jinsi ya kutekeleza katika sekta hiyo.

Alipoulizwa kuhusu ukuzaji wa sekta binafsi, Abuali amesema tayari ameshafanikisha mkutano kwa wafanyabiashara wa Tanzania na kwa sasa wanaandaa mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara wa pande mbili.

“Watakapokutana wafanyabiashara hao wa pande mbili watakubaliana maeneo ya kushirikiana na kuweka kipaumbele.”

“Kwa mfano, Palestina ina viwanda vitatu vya dawa, hivyo wafanyabiashara wa dawa wanaweza kuja kuangalia jinsi watakavyoshirikiana na Watanzania katika biashara ya dawa hiyo,” amesema. 

Chanzo: mwananchi.co.tz