Unguja. Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) leo Jumatano Agosti 14, 2019 imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali ikiwa mashine za uchunguzi wa chembe chembe za damu, vitanda, mashuka na magodoro kwa uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar.
Akikabidhi vifaa hivyo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Unguja, Mkurugenzi wa PBZ, Khadija Shamye amesema vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya Sh85.5 milioni.
Amesema PBZ imelazimika kutoa msaada huo kwa wizara ya afya kupitia hospitali zake, kutokana na sekta hiyo ni moja ya sekta muhimu inayotumiwa na wananchi wengi walio wanyonge ambao tegemeo lao ni hospitali za Serikali.
Amesema kwa upande wao watazidi kuunga mkono jitihada za wizara ya afya katika kuhakikisha suala la utoaji wa tiba bora kwa wananchi linaweza kufanikiwa siku hadi siku, kama lilivyo lengo la Serikali Kuu chini ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Halima Maulidi Salum ameupongeza uongozi wa PBZ kwa juhudi zao hizo za kusaidia sekta ya afya ambayo ni sekta muhimu katika maisha ya mwanadamu.
Amesema kati ya mashine mbili za uchunguzi wa chembe chembe wa damu walizokabidhiwa moja itapelekwa Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja na nyengine itapelekwa Hospitali ya Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo vifaa vingine ikiwa magodoro 50, vitanda 50 pamoja na mashuka 50, vitagaiwa katika hospitali za wilaya zote za Unguja.
Pia Soma
- Waliofariki ajali ya lori la mafuta Morogoro wafikia 85
- Wajumbe 32 kutoka SADC wakutana Tanzania kaujadili sekta ya afya
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi SADC
- Kitwanga anasema ataendelea kupiga kelele hadi kieleweke
“Kilichobaki sasa ni kwa madaktari husika watakabidhiwa jukumu la usimamizi wa vifaa hivyo kuwa waangalifu pamoja na kuzitunza ili kuweza kutumika kwa muda mrefu katika utoaji wa huduma kwa wananchi wetu,” amesema.