Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

PAC yashauri kukomesha foleni Daraja la Mfugale Buguruni

 103595680 Tazara2 PAC yashauri kukomesha foleni Daraja la Mfugale Buguruni

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), imetakiwa kuangalia uwezekano wa kuondoa foleni katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela (Tazara) ili mradi wa mwendokasi awamu ya tatu ukianza uwe na tija.

Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyosema kwa hali iliyopo Tazara na msongamano wa malori yanayotoka na kwenda bandarini, mradi huo ukianza hautakuwa na ufanisi endapo utakutana na changamoto za foleni katika eneo hilo kwa mabasi yake yatapita chini.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka ameeleza hayo leo Jumatano Machi 29, 2023 wakati wajumbe wa kamati hiyo, walipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT), unaonzia Posta ya Zamani hadi Gongo la Mboto kwa urefu wa kilomita 23.3.

Ujenzi wa BRT awamu ya tatu mkataba wake ulisainiwa Machi 17 mwaka 2022 unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 20 ukigharimu zaidi ya Sh230 bilioni. Mchakato rasmi wwa ujenzi ulianza Agosti Mosi mwaka 2022.

Akizungumza na wanahabari, Kaboyoka amesema “Tumeona pale (Tazara), panaweza kuwa na tatizo kubwa mbeleni, kwamba kuna mabasi ya mwendokasi yanayotakiwa kwenda haraka, hapo hapo kuna malori yanayotoka au kuelekea bandarini.

“Matokeo yake makutano yale yatazima ile dhana ya kuna mabasi ya mwendokasi na tutatengeneza foleni kubwa ya malori yatakayozuia watumiaji wengi wa barabara kuchelewa katika shughuli zao, Tanroads waangalie namna ya kutatua tatizo hili,” amesema Kaboyoka.

Kaboyoka aliyewahi kuwa Mbunge wa Same Mashariki mkoani Kilimanjaro kuanzia mwaka 2015/20, amesema endapo suala hilo halitapatiwa ufumbuzi huenda mradi wa mabasi wa mwendokasi katika barabara hiyo usiwe na maana.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila amesema maelekezo yaliyotolewa na kamati wameyachukua na watakwenda kuyafanyia kazi ikiwemo utaratibu wa kupunguza msongamano eneo la Tazara katika Daraja la Mfugale.

“Patakuwa na taa ila tunafikiria kujenga ‘fly over’ eneo la Buguruni, lakini hata pale Tazara tunaweza tukanyanyua barabara juu zaidi itakayokwenda bandarini kama ilivyo pale Ubungo (Daraja la Kijazi),”amesema Mativila.

Katika hatua nyingine, Mativila amewaambia wajumbe wa PAC hivi sasa wapo katika hatua ya kumtafuta mkandarasi atakayejenga BRT awamu ya nne kuanzia Maktaba hadi Tegeta na Mwenge hadi Ubungo yenye urefu wa kilomita 30.1.

“Ujenzi wa mradi utafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), usanifu wa kina umeshakamilika na utahusisha ujenzi wa vituo vya mabasi ya BRT,”amesema Mativila.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live