Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

PAC yaguswa na ubunifu wa Serikali mtandao

Hasunga?fit=700%2C466&ssl=1 PAC yaguswa na ubunifu wa Serikali mtandao

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), imeokoa fedha nyingi kwa kusanifu na kutengeza mifumo ya Tehama inayotumika katika taasisi za umma ambayo awali ilinunuliwa kutoka nje ya Tanzania kwa gharama kubwa.

Hasunga ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Februari 11, 2024 baada ya kamati hiyo kufanya ziara fupi ya kutembelea Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Amesema eGA imewezesha Serikali kuokoa fedha nyingi kwa kusanifu na kutengeza mifumo ya Tehema inayotumika katika taasisi mbalimbali za umma, kwani awali mifumo hiyo ilinunuliwa kutoka nje ya nchi.

Amesema uzoefu unaonyesha katika taasisi mbalimbali za umma walizozitembelea siku za nyuma kulikuwa na changamoto nyingi kuhusu suala la mifumo ya Tehama.

“Moja ya jambo lililokuwa linatusumbua sana kamati hii ni taasisi nyingi kununua mifumo ya Tehama kutoka nje, lakini msimbo (source code) zinabaki kule kwa waliotengeneza mifumo na wakati mwingine mifumo hiyo baada ya muda haitumiki tena, hivyo sisi tumekuwa tukisema hakuna thamani ya fedha katika ununuaji wa mifumo hiyo ambayo tumetumia gharama kubwa kuinunua,” amesema.

Hasunga alisema licha ya mifumo hiyo kununuliwa kwa gharama kubwa, lakini haikuwa na matokeo yaliyotarajiwa, hivyo kuziingiza taasisi hizo katika matumizi mabaya ya fedha.

“Kuna taasisi zilinunua mifumo kwa zaidi ya Sh30 bilioni, lakini mfumo haujamaliza mwaka wanautupa, na tulipowauliza walisema waliona mfumo huo haufai hivyo wameamua kutafuta mfumo mwingine,” amesema.

Amesema katika ziara hiyo kamati imebaini kwamba, e-GA imesaidia kusanifu na kutengeneza mifumo mbalimbali ya Tehama nchini ambayo imezisaidia taasisi za umma kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kununua mifumo kutoka nje ya nchi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko akizungumza wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e GOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Mjumbe wa kamati hiyo, Esther Matiko, ametaka Serikali kuwekeza zaidi kwa vijana, ili kuwezesha nchi kuingia katika teknolojia za kisasa ikiwemo ‘blockchain’ na akilii bandia.

“Uwepo wangu hapa nimepata vitu vingi vya ziada ambavyo nilikuwa sivijui, hivyo niiombe Serikali na taasisi zake wawaangalie vijana hawa na wengine ambao wapo huko nje kuhakikisha tunawasaidia na wanatumika ipasavyo katika ujenzi wa Serikali Mtandao,” amesema Matiko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema kituo hicho cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao kina eneo finyu, hivyo eGA inahitaji kutengewa bajeti ili kujenga miundombinu (majengo) yake katika eneo la Kikombo.

“Kituo chetu kinatakiwa kipate nafasi kubwa sana, mmejionea wenyewe maabara zetu ni ndogo sana, hivyo Serikali (Wizara) itakapoleta bajeti huko bungeni tunaomba mlizingatie jambo hili,” amesema Ridhiwani.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Benedict Ndomba ameishukuru kamati hiyo kutembelea kituo hicho na kuahidi kutekeleza maelekezo, maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo, ili kuimarisha bunifu na tafiti za Serikali mtandao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live