Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Opec Fund yawekeza Bilioni 500 Tanzania

Opec Fundy.jpeg Mwigulu akiwa na ujumbe toka Mfuko wa Opec

Tue, 29 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfuko wa nchi zinazozozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC FUND), umewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 218, sawa na Sh bilioni 504, kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh, ambapo walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo jijini Dodoma

Amesema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali, ukiwemo mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, mradi wa barabara ya Kazilambwa-Chagu, barabara ya Uvinza-Ilunde – Malagarasi pamoja na kufadhili mradi wa kupambana na Umasikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF.

“OPEC FUND, mmekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu katika kukuza uchumi wa nchi, kupunguza umasikini wa wananchi hasa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii watu wetu” alisema Dk. Nchemba

Amesema kuwa Serikali imeongeza kiwango cha mikopo kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia 5.1 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 5.9 mwaka 2021 na kuahidi kuwa kiwango hicho kitaendelea kuongezeka kadri hali ya uchumi itakavyoimarika, pamoja na kuendelea kuimarisha sera za kiuchumi na kifedha zitakazoendelea kujenga imani kwa wawekezaji na sekta binafsi.

Aidha, Dkt. Nchemba alitumia fursa ya mkutano huo kuliomba Shirika hilo kutoa fedha kwa njia ya mikopo nafuu na misaada kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya iliyopangwa kutekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa nyumba 10,000 za watumishi wa umma, kukuza mauzo ndani na nje ya nchi kupitia taasisi za fedha na sekta binafsi, pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tunguu – Makunduchi visiwani Zanzibar, yenye urefu wa km 48.

Aliitaja miradi mingine inayoombewa fedha kutoka Shirika hilo kuwa ni Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Songea mkoani Ruvuna, Mradi wa Maji Safi na salama wa Mafinga, mkoani Iringa na Ujenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Dawa na Vifaa Tiba, Chamazi, Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa OPEC FUND, Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh, aliahidi kuwa Mfuko wake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.

Amesema kuwa Mfuko huo umepanga pia kushirikiana na Tanzania kuisaidia sekta binafsi ili iweze kukua zaidi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji huo wa uchumi na maisha ya wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live