Ongezeko la watu katika nchi zilizopo katika bonde la mto Nile na athari za mabadiliko ya tabianchi vimetajwa kuwa tishio kwa bonde hilo.
Kutokana na tishio hilo, nchi wananchama zinazopitiwa na bonde hilo zimetakiwa kuweka mikakati endelevu utakaosimamia utunzaji na kukabiliana athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wito huo umekujwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na ongezeko kubwa la watu katika nchi zinazotegemea maji kutoka mto huo unaohudumia nchi 11, Tanzania ikiwemo.
Hayo yameelezwa leo Mei 2 na Mkurugenzi Mtendaji wa sekretatieti ya bonde la mto Nile (NBI), Sylvester Matemu wakati wa mafunzo kwa watalaam wa sekta ya maji kutoka nchi wanachama zinazopitiwa na bonde hilo.
Amesema katika kipindi cha miaka 10 zaidi ya watu milioni 30 wameongezeka katika nchi zinazotegemea chanzo hicho na kujihusisha na shughuli mbalimbali ambazo ni hatarishi kwa mazingira ya chanzo hicho muhimu cha maji.
“Mwaka 2012 kulikuwa na watu milioni 238 sasa hivi tunaongelea watu milioni 272, hili ni ongezeko kubwa na ikumbukwe kuwa eneo ni lile lile na uhitaji wa maji unaongezeka.
“Sasa kumekuwa na kuingiliana kila mmoja anaona yeye ndiye anastahili kupata kile anachokitaka matokeo ya hili ni uharibifu ndiyo sababu tunazitaka nchi wanachama kuwa makini kutunza chanzo hiki.
“Watu wanahitaji maji kwa ajili ya shughuli za viwandani, kilimo, uchumi na matumizi mengine kwahiyo hapo tunaona changamoto ya uharibifu wa mazingira na ndiyo maana tumekutana kujadiliana kwa pamoja kila nchi ichukue hatua zake kuhakikisha tunadhibiti hali hii,” amesema Matemu
Katika hilo Matemu alizitaka nchi wananchama kuweka mkazo katika sera za mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
“Ajenda ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi iwe endelevu kwetu sote maana wote tunafahamu umuhimu wa maji, hivyo tuna kila sababu ya kukilinda chombo hiki. Tulichukulie suala hili kwa uzito na liwe kwenye mikakati yetu ya kila siku, hakuna mbadala wa maji hivyo ni lazima tuyatunze kuhakikisha yanaendelea kuwepo,”
Nchi zinazopitiwa na bonde la mto Nile ni pamoja na Misri, Ethiopia, Eritrea, Kenya, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda, Sudan, South Sudan, and the Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Akizungumza kwenye mkutano Mkurugenzi wa rasilimali za maji, Wizara ya Maji, George Lugomela amesema Tanzania haitakuwa kikwazo kwa bonde la mto Nile kuendelea huku akisisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano huo baina ya nchi wanachama.
“Kutokana na hali ya siasa na uchumi wa dunia ushirikiano wetu ni nguvu madhubuti kwa lengo la kuleta maendeleo ya watu wetu kupitia sekta ya maji ambayo ni kichocheo cha uzalishaji wa sekta nyingine. Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano wa maji shirikishi kwenye ubia wa bonde la mto Nile,” Lugomela.