Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFITI), Dk Rushingisha George amesema ongezeko la asidi bahari kwenye Bahari ya Hindi nchini limekuwa likiathiri sana viumbe wanaoishi majini na maisha ya wananchi wanaotegemea rasilimali hizo.
Dk Rushingisha aliyasema hayo juzi wakati wa warsha ya kuutambulisha mradi wa kutathmini kiwango cha asidi bahari katika mkondo wa Tanga na Pemba kwa maofisa uvuvi na wadau wa bahari wilayani Mkinga.
Alisema malengo ya mradi huo ni kutaka kutambua tabia za maji kwenye mifumo ya ikolojia yao, kuangalia kama kuna mabadiliko ya tabia za maji kwenye mifumo ya ikolojia yao na nini kimesababisha.
Aidha, alisema sambamba na hilo wataweka boya katika eneo hilo ambalo litapima tabia za maji baharini kwa muda mrefu na hatimaye kuweza kupata takwimu sahihi na baadaye kuona namna ya kuboresha.
"Kwa sababu asilimia 30 ya hewa ya ukaa imekuwa ikihifadhiwa baharini na kuhifadhi hewa ya ukaa baharini tabia za maji hubadilika na kuathiri mfumo wa ikolojia na mifumo hiyo ikiharibika huduma zinazotokana na mifumo hiyo nazo zinaathirika ikiwemo upatikanaji wa samaki na mazalia ya samaki," alisema.
Alisema kupitia mradi huo wanategemea watapata takwimu sahihi ambazo watazichakata na kuangalia hali halisi ya maji yao ipoje na wanaangalia pia hatua za kuchukua ili kuziboresha na kuzipeleka taarifa hizo zitumike kwenye sera na upangaji maendeleo endelevu ya bahari.
Mtafiti huyo aliongeza kwamba mradi huo unahusisha Wilaya ya Mkinga miezi saba lakini boya ambalo wataliweka litakuwepo zaidi ya miaka 10.
"Tulishaweka boya Dar es Salaam na tutaweka maboya maeneo mbalimbali hapa nchini... Mara nyingi tunategemea wananchi watatupa ushirikiano wa kutosha kwani boya lina faida nyingi katika maisha yao," alisema.
Hata hivyo, alisema uzoefu walionao kwa mfano boya lililowekwa Dar es Salaam kwa bahati mbaya wananchi waliiba baadhi ya vifaa.
Ni kwa msingi huo alitoa wito kwa wananchi waendelee kuyalinda maboya hayo kwa sababu yanawekwa kwa gharama kubwa na ni kwa faida kubwa ya nchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Asha Churu alisema mradi huo wa kupima asidi Bahari ya Hindi wameupokea kwa mikono miwili sababu ni eneo ambalo limechaguliwa kwenye utoaji wa taarifa au takwimu za utekelezaji wa mradi huo.
Asha ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wilayani Mkinga alisema kama dunia kwa sasa inavyokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, taarifa zitakazopatikana zikichakatwa baadaye na kusambazwa kwa wana jamii zitawasaidia kujikinga na ongezeko la asidi baharini sambamba na mabadiliko mengine ya tabianchi.