Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa masoko aonya wafanyabiashara na mikataba batili

D3484c3e79c5e132b1f2b684b50b3f43 Ofisa masoko aonya wafanyabiashara na mikataba batili

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISA Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna amewataka wafanyabiashara kwenye mabanda, maduka na meza zinazomilikiwa na Halmashauri ya Jiji kutoingia mikataba batili inayowatia umaskini.

Alisema hayo kutokana na wafanyabiashara kadha kujitokeza na malalamiko ya tozo kubwa wanayoitoa kwa walioingia nao mikataba katika maeneo hayo tofauti na ile iliyoelekezwa na Halmashauri ya Jiji.

Ofisa huyo akifafanua zaidi aliwataka wafanyabiashara hao kuingia katika mikataba halali inayotolewa na kutambuliwa na halmashauri kwa watumiaji wa maeneo yake.

Wafanyabishara hao walisema wenye maduka, mabanda na meza wamejitengenezea mikataba yao binafsi inayowataka kulipa kodi kubwa tofauti na ile iliyo halali inayotolewa na halmashauri .

Akizungumza na walalamikaji hao ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao ,Yuna alisema kwa nyakati tofauti ofisi yake inaitambua mikataba inayotolewa na halmashauri na siyo ya kutengenezwa na watu binafsi.

Aliwataka wafanyabiashara hao kufanya miamala yao upya na halmashauri ya Jiji ili waweze kutambuliwa rasmi na waweze kuondokana na wizi na utapeli wanaofanyiwa na waliowapangisha.

Alisema halmashauri ya Jiji imekuwa na zoezi la kuwabaini wote waliopangisha kwenye mabanda ya maduka na meza za biashara yaliyopo ndani ya masoko ya Jiji, na kuwanyang'anya vibanda hivyo ili viweze kupangishwa kwa wengine.

"Tumekuwa na zoezi la kuwanyang'anya wale wote tunaowabaini wamepangisha wafanyabishara wengine na tunachofanya tunawapa wengine kwa kuwapa mikataba yetu ambayo ina masharti halali ya makubaliano"alisema.

Pia aliwataka wafanyabishara wanaolalamika kuendelea kutoa taarifa kwa wale waliowapangisha ambao wamekuwa wakiwaibia kwa kuwatoza kodi tofauti na iliyoelekezwa na Jiji ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Chanzo: habarileo.co.tz