Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OSHA yakamilisha tathmini Bwawa la Nyerere

Bwawa La Mwalimu Julius Nyerere JNHPP OSHA yakamilisha tathmini Bwawa la Nyerere

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umekamilisha tathmini ya awali ya vihatarishi vya usalama na afya katika eneo la mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHP) lililopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Kifungu Na. 60 cha Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, wamiliki au wasimamizi wa sehemu za kazi, wanawajibika kuhakikisha maeneo yao ya kazi yanafanyiwa tathmini ya vihatarishi vya usalama na afya walau mara moja kwa mwaka.

Lengo la tathmini hiyo ni kupata taarifa muhimu zinazohitajika, kuandaa mikakati madhubuti ya kulinda uwekezaji na kuwakinga wafanyakazi dhidi ya athari za vihatarishi katika eneo la kazi husika.

Taarifa ya kukamilika kwa tathmini hiyo imetolewa na OSHA kwa vyombo vya habari leo Machi 11, 2024 baada ya viongozi wa taasisi hiyo kufika eneo la mradi kama sehemu ya kukamilisha kazi hiyo ya tathmini.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema mwaka 2022, Shirika la Umeme (Tanesco), liliiomba OSHA kufanya tathmini ya awali ya vihatarishi katika eneo la mradi na kutoa ushauri elekezi kuhusiana na uimarishaji wa mifumo ya kudhibiti vihatarishi mahali pa kazi.

“Hivyo, baada ya wataalamu wangu kukamilisha kazi niliyowatuma, nami nimeona ni muhimu kufika katika eneo la mradi kuona kama kazi hiyo imefanyika kikamilifu. Aidha, imekuwa ni muhimu pia kuja kuona hali ilivyo baada ya mtambo mmoja kuwashwa kwani wakati tathmini inafanyika uzalishaji ulikuwa bado haujaanza,” amesema.

Mwenda amesifu hatua iliyochukuliwa na Serikali kutekeleza mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji, kwa kuwa kutachochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Akielezea mchango wa OSHA katika mradi huo, kiongozi huyo amebainisha kuwa taasisi hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi wa usalama na afya mara kwa mara tangu mradi ulipoanza na hivyo kupunguza ajali, magonjwa na vifo miongoni wa wafanyakazi wa mradi.

Ameongeza kuwa ukaguzi, miongozo na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA umesaidia kwa kiwango kikubwa mradi huo kutekelezwa kwa mafanikio, ikiwemo kukamilika kwa wakati na katika viwango stahiki kutokana na kuwa na nguvu kazi yenye afya njema na mitambo yenye ufanisi wa kutosha.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa mradi huo kutoka Tanesco, Mathew Bundala, amesema ushirikiano wao na OSHA umepunguza ajali, magonjwa na vifo vya wafanyakazi katika eneo la mradi.

Mradi JNHPP unaogharimu zaidi ya Sh6.5 trilioni ukikamilika utazalisha megawati 2,115 na kuifanya Tanzania yenye mahitaji ya megawati 1,363.9 iwe na umeme wa kutosha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live