Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OSHA na kibarua kizito makazini

F1bb7508b7fa60afffa0544252dad816 OSHA na kibarua kizito makazini

Thu, 21 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umepanga kuboresha mazingira ya uwekezaji biashara nchini kupitia uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwafanya wawekezaji wajisikie fahari kuwekeza nchini.

Hayo yalielezwa jana na Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, wakati akifungua kikao kazi cha siku tano jijini Dodoma kilichowakutanisha Wakaguzi wa Afya wa Osha kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“Wote tunaona mwelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan unavyosisitiza namna ya kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kufanya biashara nchini hivyo kupitia kikao kazi hiki sisi Osha ambao ni taasisi wezeshi tunaangalia ni namna gani ambavyo tunaweza kuwezesha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini yakawa ni rafiki zaidi hivyo kuwafanya wafanyabiashara na wawekezaji wajisikie fahari kuwekeza nchini,” alisema.

Alisema wamekaa na timu ya madaktari wa Osha wapatao 100, nia na madhumuni ikiwa ni kuhakikisha wanatoa huduma bora na kwa wakati lakini pia wanaangalia ni namna gani watawezesha maeneo ya kazi nchini yaweze kusimamia Sheria Namba 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa Osha, Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika siku za hivi karibuni limepitisha azimio la kila nchi mwanachama ahakikishe anasimamia kikamilifu masuala ya usalama na afya kazini na kwamba Osha nayo lazima ijipange kutimiza azimio hilo la ILO.

Wakaguzi wa afya wa Osha wamesema baada ya kikao kazi hicho kumalizika watakuwa na maono ya pamoja katika kuboresha mazingira ya kazi nchini huku wakitoa wito kwa ajili ya kusimamia ipasavyo Sheria Namba. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ili kuleta tija katika uzalishaji.

Mkaguzi wa Afya wa Osha, Blandina Reuben aliwataka waajiri kusimamia ipasavyo sheria na miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuleta tija katika uchumi wa nchi yetu

Chanzo: www.tanzaniaweb.live