Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nzi anavyotumika kuzalisha chakula cha mifugo

Nzi Mifugo Mifugo Nzi anavyotumika kuzalisha chakula cha mifugo

Thu, 16 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wengine wakimuona nzi ni mdudu mchafu na asiye na faida, mhadhiri wa uchumi na biashara, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Nicholaus Tutuba amebuni teknolojia inayowezesha kutengeneza chakula cha mifugo jamii ya ndege kwa kutumia nzi chuma.

Akizungumza katika wiki ya ubunifu na mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Dk Tutuba alisema ubunifu huo utawapunguzia gharama wafugaji.

Akielezea jinsi ubunifu huo unavyoweza kufanya kazi, Dk Tutuba ambaye pia ni Kaimu Meneja Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Viwanda chuoni hapo, alisema wanawachukua nzi na kuwaweka katika geji maalumu iliyotengenezwa kwa ajili ya kuwatunza na baada ya siku tatu hutaga mayai.

Alisema mayai hayo yanakwenda kuwekwa katika kifaa maalumu cha kulelewa na kugeuka mabuu (lava) ambayo hupewa chakula maalumu kwa siku nane, hivyo kuwa na ukubwa wa kutosha kwenda kumengenya takataka zilizosagwa.

Alisema baada ya kuwaweka mabuu hao katika takataka hizo wanaendelea kula kwa muda wa siku 12 hadi 20 na kuendelea kukua na kuwa funza wakubwa.

“Baada ya kuwa funza wakubwa tunawachukua na kuwakausha tunawatumia kama chakula cha mifugo, ikiwemo kuku na bata; pia tunasaga wanatumika kama chakula cha samaki,” alisema Dk Tutuba.

Akizungumza namna wanavyopata takataka, Dk Tutuba alisema takataka wanazozisaga zinatokana na mabaki ya chakula au viumbe hai (organics waste) na wanazipata katika hoteli, masoko na kwenye madampo.

“Tunachokifanya tunakwenda kukusanya taka katika hoteli, madampo na masoko kisha tunasaga katika mashine maalumu ya kusagia taka, tukimaliza tunapitisha katika joto ambalo limepimwa kuua bakteria na wadudu wengine,” alisema.

Alisema ubunifu huo unasaidia katika usafi wa mazingira kwa kuondoa takataka nyingi ambazo manispaa imekuwa ikihangaika kuzizoa kutoka katika mazalia na chakula cha mifugo jamii ya ndege.

Dk Tutuba alisema imebainika kuwa nzi hao wana kiwango kikubwa cha mafuta na protini ambacho wafugaji wamekuwa wakikipata katika damu ya mfugo, vumbi la samaki na mashudu.

“Kwa hiyo badala ya kutumia mabaki ya dagaa tunatumia haya mabuu yanayotokana na hawa nzi. Tunasema nzi ni wachafu hawana faida, lakini sisi tunaweza kutumia nzi hawa kupata faida hizi mbili,” alisema Dk Tutuba.

Pia, alisema kwa sasa wako katika utekelezaji wa mradi wa ubunifu huo na wameajiri vijana sita na kutenga eneo la eka mbili; vijana wanne wanasaidia kukusanya takataka na wengine wako katika eneo hilo la uzalishaji.

Hata hivyo, alisema bado wanahitaji maboresho katika mradi huo kwa kuwa hivi sasa wako katika ujenzi wa miundombinu.

“Aina ya nzi hawa ni wale wanaofanya decomposition (kumeng’enya) ndio maana unakuta mnyama amekufa porini hakuna nzi yeyote lakini unakuta mnyama ameoza. Kitu kimojawapo kinachofanya aoze ni hawa inzi wanaofanya decomposition,” alisema Dk Tutuba.

Alisema kwa kutumia ekari mbili hizo wana uwezo wa kuozesha taka hadi tani 140,000 kwa mwezi kama wakianza utekelezaji wa mradi huo.

Alisema lengo kubwa la ubunifu huo ni kusaidia katika usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini na lengo jingine kupata chakula cha mifugo chenye virutubisho vingi.

Dk Tutuba alisema kwa sasa asilimia 80 ya mayai yanayopatikana kutokana na ubunifu huo, wanaipeleka katika uzalishaji wa mabuu kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha mifugo, huku asilimia 20 wanakwenda kuzalisha nzi chuma ili kulinda kizazi cha nzi hao.

Alisema asilimia 10 ya takataka zinazochakatwa huwa ndio zinatoa mabuu kwa ajili ya chakula cha mifugo hao, hivyo kuozesha taka tani 140,000 kutawezesha kupata tani 10 za chakula za mifugo.

Alisema kilo moja ya mabuu wanaopatikana kutokana na nzi hao wanatumika kuchanganyia katika kilo 10 za pumba hivyo mfugaji halazimiki kuchanganya vitu vingine katika chakula.

“Kwa mfano sasa hivi wanachanganya soya, mashudu na kitu cha kuweka protini lakini imekuja kudhihirika kuwa hawa nzi wanazo hizo ingredient (virutubisho) vyote.

“Kwa hiyo hutahitaji damu kwa sababu kwenye damu tunatafuta iron (madini chuma), lakini hawa wameonekana wana kiwango kikubwa cha iron kuliko kilichoko katika damu,” alisema Dk Tutuba.

Alisema utafiti unaonyesha mabuu hayo yana kiasi kikubwa cha mafuta kuliko yaliyopo katika mashudu yote ya mimea.

Dk Tutuba alisema mabuu yanamhakikishia usalama wa mifugo mfugaji kwa sababu wataepuka matumizi ya damu ambayo wakati mwingine inakuwa na magonjwa; hivyo kuhamishia kwenye mifugo yake.

Kuhusu kiasi cha gharama kinachookolewa kwa kutumia mabuu badala ya virutubisho vingine vya chakula cha mifugo, Dk Tutuba alisema kwa sasa wanafanya utafiti katika kampuni mbalimbali za chakula cha kuku kuangalia viwango vya uchanganyaji wa chakula cha mifugo.

Alisema hiyo inatokana na kila kampuni kuwa na viwango vyao vya virutubisho wanavyoviweka wakati wa utengenezaji wa chakula hicho.

Alisema bei ya kilo moja ya mabua wanauza kati ya Sh10,000 hadi Sh15,000 kulingana na umbali wa mteja alipo ili kufidia gharama za usafirishaji.

Mhitimu wa chuo hicho, Herman Edward ambaye alishiriki katika utafiti huo alisema nzi chuma wanapatikana katika vyanzo vya maji wakati wa jua na alikwenda kuwatega kwa ajili ya kupata mbegu ya kuanza.

“Nilikuwa nawakamata kidogo kidogo na ilinichukua kama miezi minne kupata kilo moja ya nzi kwa ajili ya mbegu,” alisema Herman ambaye sasa anatumia teknolojia hiyo kufuga na mabaki ya taka hizo kama mbolea kwa ajili ya mimea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live