Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyuma ya pazia bei nafaka kupaa

Bei Za Bidhaa 4.crdownload Nyuma ya pazia bei nafaka kupaa

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wafanyabiashara wa chakula wa jumla wametaja kinachosababisha bei ya bidhaa hiyo kupanda mara kwa mara licha ya serikali kuweka juhudi mbalimbali kuidhibiti.

TEMEKE

George Mashaka (45), mfanyabiashara wa mchele kwa jumla katika Soko la Temeke, alisema kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kunachangia mfumuko wa bei ya vyakula, pia upatikanaji wa bidhaa hiyo umekuwa mgumu kwa sasa kutokana na wakulima wa ndani kuangalia zaidi masoko ya nje ya nchi kwa ajili ya maslahi yao.

Alisema kwa sasa mchele ulipaswa kuuzwa kwa bei ya chini kwa kuwa ni miezi ya mavuno, akirejea kumbukumbu zake za miaka miwili iliyopita kipindi kama hiki bidhaa hiyo ilikuwa inapatikana kwa bei ya kuanzia Sh. 1,200 kwa bei ya jumla, lakini sasa wanauza kuanzia Sh. 1,800 kwa kilo.

Mfanyabiashara huyo alisema kwa sasa wanalazimika kununua mchele huo kwa gharama sawa na wanunuzi wa nje ya nchi kwa kuwa bila kufanya hivyo, bidhaa zote zitakwenda kwenye nchi zao, zikiwamo Kongo, Rwanda, Burundi na Uganda na wao kutofanya biashara.

"Soko hili sasa hivi limevamiwa na wafanyabiashara kutoka nchi za nje. Ukienda sasa hivi Mbeya, utakuta wafanyabiashara wa Kongo wamejaa, ukienda Mpanda na Kanda ya Ziwa, unakuta wafanyabiashara kutoka Burundi na Uganda wamejaa, ambao sasa hivi wanakwenda moja kwa moja shambani kununua mpunga badala ya kwenda kwenye mashine.

"Tena kama wewe ulikuwa unanunua gunia kwa Sh. 40,000, mwenzako ananunua kwa Sh. 60,000. Sasa mkulima si atamuuzia Mganda?" George aliwasilisha uzoefu wake.

Alisema hali hiyo imesababisha wafanyabiashara wa ndani kupandisha bei ya bidhaa hizo, huku akikiri biashara yao hiyo kwa sasa ni ngumu kwa sababu wamepoteza wateja, na katika kukabiliana nayo, wanalazimika kuuza kwa bei ya rejareja ili kufikia malengo yao.

“Zamani tulikuwa tunauza mchele kuanzia kilo 10 kwa kuwa tulikuwa tunauza Sh. 1,200 hadi 2,000 kwa kilo, lakini sasa jeuri hiyo baadhi yetu hatuna. Ni kwa sababu mchele huo huo tunauza kwa Sh. 1,800 hadi 2,500, wateja wamepungua. Kwa hiyo, sasa akija mtu akitaka kilo moja tunamuuzia, mradi na sisi tupate riziki," alisema.

Mfanyabiashara wa jumla wa maharagwe katika soko hilo, Rashid Ahmad, alisema mbali na soko la bidhaa hizo kuvamiwa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, mwaka huu mavuno yamekuwa kidogo na upatikanaji wake umekuwa wa shida na wakulima kupandisha bei ili kupata faida zaidi.

Ahmad alisema kupanda kwa gharama za usafirishaji pia kumekuwa kikwazo kwao, hivyo wanalazimika kupandisha bei ili kufidia ongezeko la gharama za usafirishaji.

"Hawa wenzetu (nchi jirani) inaonekana mwaka huu kama hawakulima kabisa kwa sababu wamejaa sana nchini na wananunua kwa bei ya juu tofauti inayotambulika.

"Kwa hiyo, inabidi na sisi tufike bei hiyo ili tupate bidhaa, lakini itambulike pia kwa sasa kusafirisha gunia la kilo 100 kutoka Makambako hadi hapa Temeke ni Sh. 10,000 kutoka Sh. 6,000 ya awali. Sasa hatuna jinsi, lazima na sisi tupandishe bei," alifafanua.

SHINYANGA

Mfanyabiashara Alex Paulo wa mkoani Shinyanga, aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki kuwa kilo moja ya maharagwe kwa sasa wanaiuza Sh. 2,400 kwa kuwa wananunua gunia la kilo 100 kwa Sh. 220,000 tofauti na awali bei ilikuwa Sh. 160,000 hadi 170,000.

Wakati bei ikiwa juu kwenye baadhi ya maeneo nchini, mfanyabiashara wa unga wa mahindi kwa bei ya jumla katika Soko la Tandale aliyejitambulisha kwa jina la Big, alisema kwa sasa bidhaa hiyo imeanza kupatikana kwa wingi na wameshuhudia kushuka kwa bei na anaamini kama hali hiyo itaendelea, gharama zitarudi kama zamani.

"Tuna wiki sasa mahindi yameanza kuja kwa wingi, kidogo gharama zimeshuka huko tunakonunulia na sisi tumeshusha. Sasa hivi kiroba cha kilo 25 tunauza Sh. 35,000 kutoka Sh. 38,000.

"Kiroba cha kilo 10 tunauza Sh. 15,000 kutoka Sh. 17,000 na kilo tano tunauza Sh. 7,000 kutoka Sh. 8,000 tuliyokuwa tumefikia hivi karibuni," alifafanua.

Hali hiyo ni tofauti kulinganisha na baadhi ya mikoa ikiwamo Arusha, mahindi yameonekana bado yanauzwa bei juu.

ARUSHA

Elizabeth Mafwere, mfanyabiashara katika Soko la Kikatiti lililoko wilayani Arumeru mkoani Arusha, alisema kwa sasa wananunua gunia la mahindi kwa Sh. 100,000 na wao wanawauzia wanunuzi wa jumla kwa Sh. 105,000, akifafanua kuwa ni ongezeko kubwa kulinganishwa na miaka iliyopita.

“Tulizoea msimu huu wa mavuno na mahindi yakiwa mapya gunia tulinunua kwa Sh. 30,000 hadi Sh. 40,000, hali imekuwa ni tofauti sana mwaka huu, kwa sasa ndio kwanza wakulima wanaanza kuvuna kile kidogo alichopatikana," alisema Mafwere.

Alphonse Charles, dalali wa mchele jijini Arusha, alisema kuwa kitendo cha wafanyabiashara wa nje kununua bidhaa kwa wakulima kwa bei ya juu, bei  inakuwa juu kwa sababu hata wanunuzi wa ndani nao wanakwenda kufuata bidhaa hiyo mikoani kwa wakulima.

"Ina maana bei kule kwa wakulima inapopanda, inabidi na sisi huku tuje kupandisha, na hawa nao wamekuwa wajanja, sasa hivi wanakwenda wenyewe mashambani au mashineni huko kununua mchele, sasa hapo na sisi pia tunaathirika maana wateja wamepungua sana," alilalamika.

TANGA

Mkoani Tanga, Nipashe imeshuhudia katika baadhi ya maeneo unga wa ngano umepanda kutoka Sh. 1,500 kwa kilo hadi Sh. 2,000 huku unga wa mahindi nao ukielezwa kupanda kutoka Sh. 1,000 kwa kilo mpaka Sh. 1,500.

Katibu wa Soko Kuu la Mgandini jijini Tanga, Shabani Mohamed, alisema magari yaliyokuwa yakipeleka bidhaa kwenye soko hilo, yamepungua kutokana na bidhaa kupanda bei na kusababisha baadhi ya bidhaa kuadimika.

DODOMA

Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma, Meneja wa Soko la Kimataifa la Mazao la Kibaigwa mkoani Dodoma, Emanuel Kereyani, alisema msimu huu bei ya mazao hasa mahindi imepanda hadi kufikia Sh. 820 kwa kilo kwa sasa.

"Bei ya mahindi kwa sasa inapanda badala ya kushuka. Wakati msimu ulipoanza, kilo moja ilinunuliwa kwa Sh. 600 lakini sasa yanapanda tu, yamefika Sh. 820 kwa kilo kwa saa na kuna wakati yalifika hadi Sh. 900 kwa kilo lakini baadaye yalishuka na kufikia hii Sh. 820," alisema.

Kiongozi huyo alisema alizeti kilo moja sasa inauzwa Sh. 1,000, mtama mweupe na mwekundu gharama yake ni Sh. 620 hadi 650 kwa kilo.

"Hizi bei tukilinganisha na misimu iliyopita zipo juu sana, tangu soko lianzishwe haijawahi kutokea, mwaka huu bei ni kubwa sana, misimu mingine iliyopita kilo tulikuwa tunanunua hata kwa Sh. 350," alisema.

Nipashe ilipohoji kuhusu wafanyabiashara wa nje kununulia mazao mashambani, meneja huyo alikiri kuwapo hali hiyo, akisema wameingia kwa kasi huko vijijini na wananunua kwa bei kubwa.

"Kwenye soko letu hatuna uhaba mkubwa kwa sababu mazao yanaingia kila siku, kwa sasa tupo kwenye msimu wa mahindi, yanaingia kwa wingi lakini bei imekuwa kubwa," alisema.

Mwenyekiti wa Soko Kuu la Majengo jijini Dodoma, Godson Rugazama, alisema hali ya upatikanaji wa mazao katika soko hilo ni mbaya huku bei zikiendelea kupanda kila siku.

Alisema kiroba ya unga wa mahindi cha kilo 10 ambacho mwaka jana kipindi kama hicho kilikuwa kinaunzwa Sh. 17,000, mwaka huu kinauzwa Sh. 38,000, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya bei ya mwaka jana.

MIKAKATI NFRA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa, alisema wakala unaanza kununua mahindi kwenye mikoa mbalimbali na kwamba bei itazingatia hali ya mikoa husika.

Alisema wamepanga kununua tani 100,000 za nafaka. Kati yake, mahindi tani 95,000, mpunga tani 4,000 na mtama tani 1,000.

Alisema na wanakwenda kununua katika mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ndiyo ina chakula kwa wingi, huku akikiri uzalishaji wa mwaka huu umeshuka kulinganisha na ule wa mwaka jana.

Ofisa huyo alisema kuwa kabla ya kununua, wanajiridhisha kwanza kuhusu usalama wa chakula nchini.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alipowasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, alitaja vipaumbele vyao ikiwa ni pamoja na kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula ndani ya nchi na kuuza nje ya nchi.

Bashe pia alisema watafanya mwelekeo wa uzalishaji wa mazao ya chakula kuwa wa kibiashara, akibainisha kuwa wataongeza mauzo ya mazao nje ya nchi  kutoka Dola za Marekani bilioni 1.2 hadi Dola za Marekani bilioni tano ifikapo mwaka 2030.

MBEYA

Mkoani Mbeya, Nipashe ilitembelea masoko mbalimbali ya Jiji la Mbeya na yaliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi kwa ajili ya kuangalia bei za mazo hayo na upatikanaji wake ambapo wafanyabiashara wa mazao hayo walisema kwa sasa kila zao limepanda bei.

Katika Soko la Mbalizi mahindi yanauzwa kwa bei ya kati ya Sh. 13,000 na 15,000 kwa debe, huku wafanyabiashara wakieleza kuwa upatikanaji wa nafaka hizo ni wa shida kwa sasa.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Rhoida Sanga alisema licha ya bei ya nafaka hizo kuwa nzuri kwa sasa, lakini wakulima wengi hawapeleki kwenda kuuza wakisubiri ipande zaidi na kwamba baadhi yao walivuna kidogo hali ambayo inawafanya wasiuze.

Alisema miaka mingine kipindi kama hiki ambacho wakulima wengi wanakuwa wametoka kuvuna walikuwa wananunua kwa bei ya kati ya Sh. 4,000 na 6,000 kutokana na kuwa mengi, lakini mwaka huu ni tofauti.

“Mwaka jana kipindi kama hiki tulikuwa tunanunua debe moja Sh. 5,000 na kuuza 6,000, lakini mwaka huu tunanunua Sh. 13,000 mpaka 14,000 na tunauza Sh. 15,000 lakini bado hayaonekani,” alisema Rhoida.

Naye Sophia Mwakagali, ambaye ni mfanyabiashara wa maharagwe alisema kwa sasa wananunua kati ya Sh. 28,000 na 38,000 kwa debe kulingana na aina ya mbegu na ubora wa mazao yenyewe.

Alisema baadhi ya maharagwe yakiwamo aina ya Kigoma yanauzwa bei kwa sababu yanahitajika zaidi sokoni kutokana na kutumiwa na watu wote wakiwemo hata wenye vidonda vya tumbo.

Alisema maharagwe ambayo yanauzwa bei ya chini ni Rosekoko ambayo ndiyo wananunua Sh. 28,000 na kwamba wao wakiuza huwa wanaongeza kati ya Sh. 1000 na 2000 ili wapate faida.

Katika baadhi ya mashine za kukoboa mpunga na kulikutwa mchele ukiuzwa kati ya Sh. 35,000 na 42,000 na wafanyabiashara walisema bei hizo hutofautiana kulingana na aina ya mpunga na kiwango cha ubora baada ya kukobolewa.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Salome Mzopola alisema mwaka huu mpunga sio mwingi kama ambavyo inakuwa miaka mingine kutokana na mvua kuisha mapema hasa katika Bonde la Kamsamba wilayani Momba ambako ndiko wanatoa asilimia kubwa ya mpunga unaouzwa Mbalizi.

*Imeandaliwa na na Jenifer Gilla (Dar), Richard Makore (Mwanza), Allan Isack, Tumaini Mafie (Arusha), Jaliwason Jasson (Manyara), Oscar Assenga (Tanga),  Restuta Damian (Bukoba), Happy Severine (Simiyu), Marco Maduhu (Shinyanga), Renatha Msungu Paul Mabeja (Dodoma), na Nebart Msokwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live