Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyanda za Juu waonyeshwa fursa za kilimo cha mazao lishe

5230 MAHINDI Nyanda za Juu waonyeshwa fursa za kilimo cha mazao lishe

Fri, 10 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKULIMA wa Mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wameshauriwa kuchangamkia kilimo cha mazao lishe ambayo yamefanyiwa utafiti.

Mazao hayo yamefanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Kituo cha Uyole jijini Mbeya ambayo ni kwa ajili ya chakula na biashara.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk. Tulole Bucheyeki, alisema wamezalisha mbegu za kutosha za mazao lishe ambayo ni mahindi, maharage na viazi ambayo yana virutubisho vya kutosha kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto.

Alisema mazao hayo yanastawi vizuri katika mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo kiwango cha udumavu kwa watoto kipo juu kuliko hata maeneo ambayo hayazalishi chakula kwa wingi.

“Mazao haya yana soko kubwa sana, lakini mbali na kuwa na soko pia yanatumika kwa ajili ya chakula, na yana vitamini ambazo ni muhimu kwa ajili ya kukabiliana na udumavu kwa watoto, tusisubiri watoto wapate shida ndio tuanze kutafuta dawa,” alisema Dk. Bucheyeki.

Aliwataka wananchi wanaohitaji kulima mazao hayo kwenda kwenye taasisi hiyo ili wapate mbegu na wakapande kwenye maeneo yao na kwamba watapewa elimu ya kilimo cha kisasa cha mazao hayo.

Dk. Bucheyeki pia alisema wameandaa mashamba darasa kwenye mashamba ya taasisi hiyo ambayo wanayatumia kufundishia wakulima kilimo cha kisasa, na chenye tija hivyo kila anayehitaji elimu hiyo anafundishwa kwa vitendo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live