Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyamapori kichocheo cha ukuaji uchumi

F8c0913058808480fc9c1b8975ddf49e Nyamapori kichocheo cha ukuaji uchumi

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MOJA ya mambo ya msingi katika taifa lolote duniani ni kuwawezesha wananchi wake kuwa sehemu ya kumiliki, kutunza rasilimali zake ili ziweze kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Kwa nchi yenye uchumi wa kati kama Tanzania, uamuzi huo ni wa msingi zaidi kwani unaiwezesha jamii kubwa kunufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi yake, kwa kukutana nazo kwenye ujenzi wa miundombinu bora, vituo vya afya, shule na taasisi za elimu ya juu kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wake kupata elimu bora.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine katika Bara la Afrika nayo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wananufaika vyema na rasilimali zake na mapato mengine ya nchi yanayopatikana kwa ajili ya ustawi wa maisha yao na pia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Ni kwa mantiki hiyo basi, hivi karibuni Serikali katika kuhakikisha wananchi wake wananufaika na rasilimali zake za wanyamapori nchini, imetangaza rasmi kwa wafanyabiashara wote kuanzisha maduka (bucha) maalum za kuuza nyama pori.

Uamuzi huo umepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wengi katika maeneo mengi ya nchi, huku baadhi yao wakipongeza uamuzi huo wa serikali wa kuanza kuruhusu wananchi kunufaika na rasilimali za wanyama wa porini.

Akizungumza hivi karibuni jijini Mwanza kwenye kikao kazi kwa wafanyabiashara wa bucha kwa ajili ya kutoa elimu ya uanzishaji wa biashara ya nyama pori, Ofisa Uhamasishaji wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili Kanda ya Ziwa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Laurent Yohana anasema uanzishwaji wa biashara ya kuuza nyama pori ni mkakati mahususi wa serikali kuwawezesha wananchi kunufaika na rasilimali zao.

“Biashara hii itakuwa pia ni chanzo kikuu cha mapato kwa wananchi na serikali, kupunguza umasikini na kukuza uchumi wao,” anasema Yohana.

Anasema biashara hiyo iliyoruhusiwa rasmi na Serikali inafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni za biashara ya nyama pori za mwaka 2020.

Yohana anasema ili mfanyabiashara aruhusiwe kwa mujibu wa sheria kufanya biashara hiyo ni lazima azingatie sheria hiyo na kanuni zake na miongozo na taratibu mbalimbali zilizowekwa na Tawa.

Anasema Tawa tayari imetoa muundo wa aina za bucha mbili, bucha ya jengo maalumu na bucha ya kutembea (ya gari) ambazo ndizo zimeruhusiwa kwa wafanyabiashara kuzitumia kufanyia biashara hiyo.

“Mfanyabashara wa nyama pori atakayeruhusiwa kufanya biashara hii ni yule aliyekidhi matakwa ya sheria zinazohusiana na biashara ya uuzaji wa nyama,” anasema na kuongeza kuwa mfanyabiashara anatakiwa kulipia Sh 250,000 katika kipindi cha miaka mitano kama ada ya usajili wa bucha yake.

Hali ya uhifadhi Yohana anasema Tanzania ina wanyamapori wa aina mbalimbali, ambao wanatosha kwa watu wanaohitaji kuwekeza kwenye biashara hiyo.

Anasema kuwepo kwa utoshelevu huo wa wanyamapori hapa nchini, kunatokana na nchi kuwa na uhifadhi wa wanyamapori unaosimamiwa na sheria hiyo ya kuhifadhi wanyamapori ya mwaka 2009.

Anasema uhifadhi huo pia umesaidia uboreshaji wa miundombinu na huduma za jamii, ajira za kudumu na za muda mrefu, kuimarika na kuendeleza utamaduni wa makabila mbalimbali, kupata chakula kwa jamii na kuimarika kwa uhifadhi wa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.

Biashara ya uuzaji nyamapori Yohana anasema biashara hiyo ambayo kwa sasa imeanzishwa rasmi hapa nchini, inafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni za biashara ya nyamapori za mwaka 2020.

Anasema nyama pori ni miongoni mwa nyara ya Serikali. Anasema mtu yeyote anayetaka kujishughulisha na biashara ya nyara kama vile kuuza nyama pori kwenye bucha kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.

Pamoja na sheria hiyo na kanuni zake, pia anapaswa kuzingatia Kanuni za Uwindaji wa Wenyeji zote za Mwaka 2010, miongozo na taratibu mbalimbali zilizowekwa na Tawa.

Nyamapori kuuzwa buchani Yohana anasema nyama pori ya kuuzwa buchani inaweza kupatikana kwenye uwindaji wa wenyeji ambapo leseni ya uwindaji itatolewa kupitia ofisa wanyamapori wa halmashauri husika.

Kwa upande wa uwindaji wa kitalii, anasema nyama pori inaweza kupatikana kwa makubaliano kati ya mhitaji (mfanyabiashara) na mmiliki wa kitalu cha uwindaji wa kitalii.

“Inapatikana pia kwa kuvunwa kwenye bustani, mashamba na ranchi za wanyamapori,” anasema Maeneo yaliyotengwa Anasema mara baada ya Serikali kutangaza kuanzishwa kwa bucha za wanyamapori, agizo hilo lilikwenda sambamba na utengaji wa maeneo kwa ajili ya uwindaji wa kienyeji.

Anayataja maeneo hayo kuwa ni Kitwai Kusini-Simaniro-Manyara, Kilwa Kaskazini (Kilwa Open Area)–Kilwa-Lindi, Kisarawe (Open AreaNorth)-Kisarawe-Pwani, Ugalla Niensi- Mlele-Katavi, Simbanguru –IgwemadeteManyoni-Singida na Ipemba Mpezi-Sikonge-Tabora.

Maeneo mengine ni pamoja na Talamai-MonduliArusha na Msitu wa Matundu ulioko Iringa (Southern Highland zone).

Taratibu za kufuatwa Anasema ili mtu aweze kufanya biashara hiyo ya nyama pori kwanza anatakiwa awe na bucha inayokubalika, ambapo kimsingi anasema kuna aina mbili za bucha, bucha ya jengo maalum na bucha ya gari inayotembea.

Anasema ili mfanyabiashara aweze kuanzisha bucha, anatakiwa aandae andiko la biashara (mradi) ambalo linajumuisha aina ya nyama pori itakayouzwa kwenye bucha yake (mbichi au iliyoongezewa thamani), eneo ambapo bucha itakuwepo, picha ya muundo na muonekano wa bucha hilo (gari au jengo).

Mahitaji mengine yanayohitajika kwa mujibu wa Yohana ni kuwa na mtaji utakaowekezwa kwenye biashara hiyo na aoneshe wateja wake (mama lishe, mahoteli na watu wa kawaida) na mchanganuo wa fedha iliyowekezwa na matarajio yake ya mapato.

“Utakuwepo utaratibu wa udhibiti wa manunuzi na mauzo ya wanyamapori, lazima mfanyabiashara awe na Ledger book na mashine ya kielektroniki (EFD),” anasema.

Anafafanua kuwa iwapo biashara itahusisha uchinjaji na uchunaji lazima kwenye mchanganuo huo wa biashara uoneshe utaratibu mzima wa kuanzia kwenye vyanzo (bustani, mashamba na ranchi za wanyama)

Anasema ili mfanyabiashara ajaze fomu ya maombi ya kupata usajili na leseni ya kuuza nyama pori, lazima ajaze daraja sahihi la biashara hiyo ambalo ni daraja la pili.

“Aambatanishe na risiti ya malipo ya ada ya Sh 5000 bila kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na abainishe umiliki wa hisa kwa biashara ya ushirikiano wa Mtanzania na raia wa kigeni, hisa za Mtanzania lazima ziwe 51 na kuendelea,” anaeleza.

Anasema pia lazima aambatanishe nakala ya hati ya kibali cha kodi/hati ya idhini ya ushuru iwapo mwombaji ni bodi ya ushirika na aambatanishe nakala ya cheti cha usajili wa bodi.

“Mwombaji lazima awe ametimiza matakwa ya kisheria zinazohusiana na biashara ya nyama pori, ikiwemo kupata vibali vya afya kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS),” anasema.

Wanyama walioruhusiwa kuvunwa Anataja baadhi ya wanyama walioruhusiwa kuvunwa na kuchinjwa kwenye biashara hiyo na bei zao kwenye mabano kuwa ni nyati dume (Sh 100,000), pongo dume, nguruwe pori dume na swala granti dume (Sh 40,000) kila mmoja, pofu mbunju dume (Sh 150,000), digidigi (Sh 10,000) na swala tomi (Sh 25,000) kila mmoja.

Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye bucha jijini Mwanza, Joshwa Machage anaishukuru Serikali kwa kutoa fursa hiyo adimu kwa wafanyabiashara itakayopunguza gharama za ng’ombe na kuinua vipato vyao.

“Kwa hivi sasa ng’ombe mwenye kilogramu 150 tunamnunua kwa shilingi 1,300,000 kwa kweli tunamshukuru sana Rais John Magufuli kwa kuona ni vyema na sisi tunufaike na fursa hii ya biashara ya nyamapori,” anasema Machage.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba anawataka wafanyabiashara wenye mabucha kuchangamkia fursa za kuuza na kufanya biashara ya kuuza nyama pori.

“Serikali imetangaza rasmi kuingia kwenye uchumi wa kati kutokana na kukidhi vigezo muhimu vya kiuchumi na vile vya ulinzi na usalama na kwamba lazima wananchi watumie fursa mbalimbali kwa ajili ya kujipatia kipato,” anasema Bucha ya nyamapori ya mfano iliyozinduliwa hivi karibuni jijini Dodoma.

Chanzo: habarileo.co.tz