Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Norway yatoa Sh22.54 bilioni kusaidia kilimo

Fedha Ed Norway yatoa Sh22.54 bilioni kusaidia kilimo

Thu, 7 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Norway imetoa msaada wa zaidi ya Sh22.54 bilioni kwa Tanzania kwa ajili ya kusaidia uendelezaji wa sekta ya kilimo ambapo zitaelekezwa katika kuimarisha usambazaji wa mbolea.

Hatua hiyo inatokana na majanga yalizozikumba nchi zinazoendelea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na vita vya Russia na Ukraine vilivyoweka mazingira magumu ya upatikanaji wa chakula, mbolea na pembejeo.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 6, 2023 mara baada ya kutembelea ofisi za kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, Kurasini Dar es Salaam, Waziri wa Uhusiano wa kimataifa na Maendeleo wa Norway, Ane Beathe Tvinnereim alisema wanaamini msaada huo utaleta mabadiliko katika sekta ya kilimo.

“Nimekuja Tanzania kuhudhuria mkutano wa Mifumo ya Chakula Tanzania (AGRF), ambapo tunajadili upatikanaji wa chakula. Tunajua kuna upungufu wa chakula kutokana na majanga likiwemo vita Russia na Ukraine vinavyosababisha pia ukosefu wa pembejeo"

Alisema “Kutokana na hali hiyo Norway inatoa zaidi ya dola za Marekani 9 milioni kwa ajili ya kusaidia wananchi kupitia Mfuko wa kusaidia Kaya Masikini (Tasaf) na kusaidia kupatikana kwa usalama wa chakula,” alisema Waziri huyo.

Alisema fedha hizo pia zinakwenda kusaidia kukabiliana na majanga yatokanayo ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa ukame, au mvua kuwa nyingi, kwa hiyo fedha hizo zitasaidia kujenga miundombinu ya maji, mabwawa ili wanyama wapate maeneo ya kunywa maji na kuongeza uzalishaji wa chakula,” alisema.

Akizungumzia ziara hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde alisema imekuja ikiwa ni sehemu ya mikutano ya AGRF kwa lengo la kuangalia uwezeshaji wa mifumo ya chakula.

“Sisi Serikali kupitia Wizara ya Kilimo tunaihakikishia kampuni ya Yara ambao ni wasambazaji wa mbolea nchini, kuwa tutawapa ushirikiano kwa sababu wanasaidia sera ya Serikali katika kuinua kilimo nchini,” alisema.

Katika mazungumzo yao wamejadili namna kampuni hiyo itakavyoanza uzalishaji wa mbolea nchini. moja ya mambo tuliyojadili ni pamoja na uzalishaji wa mbolea nchini.

“Uzalishaji ni mchakato na kuna mikakati ya muda mfupi na mrefu, kwa hiyo mkakati wa muda mrefu ni pamoja na kujenga kiwanda na mkakati wa muda mfupi ni kusambaza mbolea.

“Wizara ya Kilimo imepanga kuongeza usambazaji wa mbolea nchini, ndiyo maana usambazaji wa mbolea unaanza mwezi huu ili iwafikie wakulima haraka,” alisema.

Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Yara International, Sven Tore Holsether aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuonyesha ushirikiano tangu walipoanza kazi nchini mwaka 2004.

“Lengo letu ni kuimarisha upatikanaji wa chakula ndiyo maana tunazalisha mbolea yenye virutubisho vinavyotakiwa mwilini,” alisema. Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na madhara yaliyoletwa na vita vya Russia na Ukraine, watahakikisha upatikanaji wa mbolea unaimarishwa ili kuwezesha upatikanaji wa chakula.

Neema kwa wafugaji

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa na washiriki wa mkutano wa AGRF, alisema kati ya Septemba na Oktoba, Serikali itaanzisha kampeni ya kuchanja mifugo.

“Kwa sasa tuna viwanda vya chanjo, kimoja kipo Kibaha (Pwani), kingine kipo Morogoro, kwa hiyo tunanza. Tumeshazungumza na wakuu wa mikoa,” alisema.

Awali akizungumzia katika mada ya kwanza, Ulega aliwataka vijana wanaotaka kuwekeza kwenye ufugaji na uvuvi, kufika Wizarani na kujisajili kwenye dawati la sekta binafsi.

Akizungumza ka mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliwataka wawekezaji katika sekta ya mifugo kuandaa mashamba ya malisho ili kuepuka usumbufu.

Bashe alizungumzia kero ya upatikanaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya kupata malisho, akisema kwa hali ya sasa ya uzalishaji ni vigumu kutoa chakula kwenye hifadhi ya Taifa na kuwapa wafugaji.

“Hivi karibuni wakati mambo yamekuwa magumu, kwa miaka minne tangu nimeanza kukaa kwenye Wizara ya Kilimo, niilipokea barua kutoka kwa Ulega, akiniambia anaomba tani kadhaa za mahindi, nikamwambia rafiki yangu, watu wa Longido hawana chakula, nakupaje hayo mahindi?

“Kwa hiyo yeyote anayehitaji chakula kwa ajili ya mifugo, njoo sasa tuingie mkataba kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo,” alisema.

Akisisitiza kuhusu uzalishaji wa malisho, Bashe alisema juzi waliingia mkataba na kampuni kutoka Saudi Arabia waliyoipa ekari 5,000 kuzalisha mimea ya alfaalfa.

“Mimi ni mfugaji, nikawauliza kuna wafugaji wengi hapa, kwa hiyo asilimia 50 mnabakiza ndani na asilimia 50 mnasafirisha nje,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live