SERIKALI ya Norway imesema itaendeleza ushirikiano kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Tanzania kwa ujumla ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50.
Balozi wa Norway Nchini, Tone Tinnes amesema hayo kwenye mazungumzo yake na Menejimenti ya Chuo Kikuu SUA chini ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda.
Balozi Tone alifurahishwa na kile kinachofanyika kwenye chuo hicho ikiwemo kuelimisha watu hususani wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi, kufundisha watu juu ya kilimo bora na cha kisasa hususani kilimo biashara.
Katika ziara hiyo Balozi Tone ametembelea miradi mbalimbali iliyopo chuoni hapo iliyofadhiliwa na Nchi ya Norway, ikiwemo Kituo cha Taifa cha Kuratibu Hewa Ukaa na Kituo cha Kujifunzia Kilimo Atamizi cha Kilimo Biashara.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho Profesa Chibunda amesema kuwa ziara hiyo ya Balozi Tone ni matokeo ya Mkataba wa Makubaliano uliosainiwa baina ya SUA na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maisha cha Norway ‘Norwegian University of Life Sciences.’
Makubaliano hayo yamelenga katika Sekta ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi lakini pia kuweza kufanya tafiti mbalimbali.
Profesa Chibunda amesema makubaliano hayo yamelenga pia katika kubadilishana uzoefu kati ya Vyuo hivyo ikiwemo wataalam mbalimbali wa Vyuo Vikuu, Walimu, Wanafunzi pamoja na Watafiti.