Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njia za kupata utajiri kijasiriamali

FEDHA Njia za kupata utajiri kijasiriamali

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: mwanachidigital

Watu wengi huwa wanatamani kutajirika lakini ukichunguza ni wachache wanaofikia ndoto hizo. Leo nataka tujiulize ni kwa nini wengi wanashindwa kufikia lengo hilo?

Katika mada kadhaa zilizopita niliwahi kuzungumzia juu ya makosa mbalimbali ambayo mjasiriamali anafanya na hatimaye kumuathiri kifikia katika hatua ya mafanikio aliyokusudia.

Tumejadili pia mara kadhaa watu wanavyofanya makosa katika kufanya maandalizi ya mipango ya kuingia biashara mpya, utekelezaji wa programu yake na namna kutumia muda vizuri.

Lakini pamoja na kufuata mipango mizuri ya kazi, kuna mambo ambayo mtu anapaswa kujiwekea kama misimamo yake ya kwenda mbele ama kutajirika.

Kanuni za biashara na uchumi zinaainisha mambo kadhaa ambayo kama mtu anataka kutajirika atapaswa kufuata kama kanuni au falsafa kadhaa. Miongoni ni kama zifuatazo:

Mafanikio mazuri ni yale ambayo mtu anakua kidogokidogo. Mtu ambaye amepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, lazima ipo siku atarudi nyuma. Maana ile fedha hakuipata kwa hatua zile za kukua.

Watu wengi wanapenda kuwa matajiri lakini wanataka kufikia malengo hayo kwa njia ya mkato. Fedha ya namna hiyo haiwezi kumfanya mtu akawa tajiri wa kudumu.

Kwa mfano, katika historia yangu, nikiwa natafuta maisha niliwahi kushinda tuzo kwa kuweka mipango mizuri ya kibiashara. Kuna wakati nilishinda Sh30 milioni na wakati mwingine Dola 6,000 za Marekani sawa na Sh12.6 milioni.

Katika miaka hiyo ya 2010, zilikuwa ni fedha nyingi lakini sikuzifanyia kitu chochote cha maana. Nilishangaa katika kipindi cha muda mfupi zimeisha. Unajua ni kwa sababu gani? Kwa wakati huo sikujua nini kilifanya ziishe katika muda mfupi tena bila kuona zimenifanyia jambo ambalo naweza kusema ni la msingi.

Baada ya kukua kijasiriamali kwa maana ya kufahamu kanuni za mambo ya fedha, shughuli za kibiashara nilibaini hazikuwa na faida kwangu kwa sababu wakati huo nilikuwa sijaiva vizuri kijasiriamali.

Ukizungumza na vijana wengi mitaani utasikia wakieleza kwamba wangepata milioni kadhaa, wangetangaza kufaulu kimaisha. Lakini ukweli hata ukimpa hizo fedha zinaweza kabisa zisimsaidie chochote kwa sababu hana mipango mizuri.

Mtindo wa watu wanaotaka fedha za haraka ni sawa na nyama ambayo siyo nzuri kuliwa ikiwa mbichi. Nyama iliyoiva ni sawa na yule mjasiriamali aliyekua kidogokidogo hadi kufikia hatua ya juu, ambapo wakati huo anakuwa ameimarika. Ukweli ni kwamba watu wengi hawapati maendeleo kwa sababu wanaogopa kuingia kwenye tanuru la moto ili waive na baadaye wawe wamekua vizuri kijasiriamali.

Mafanikio lazima yawe hatua kwa hatua. Lazima uungue na kupitia tanuru la moto ambalo litakuchoma taratibu mpaka utakapokamilika na kuiva kwa ajili ya kuliwa mezani. Watu wengi wanataka kufanikiwa lakini wanaogopa kupita kwenye tanuru na hufikiria njia za mkato na wengi huishia maisha ya majuto.

Ndiyo maana watu wengi wanaopata fedha nyingi ghafla huwa hawawezi kudumu nazo kwa muda mrefu. Hutumika katika muda mfupi na baadaye hurejea tena kwenye umaskini.

Mafanikio bila maumivu, wala huwezi kuona raha yake. Ukipita kwa njia ya mkato unafika kileleni lakini ipo siku mfumo unabadilika na anguko lake litakuwa kubwa, matokeo yake huwezi kurudi tena juu.

Mtu ambaye amepata mafanikio kwa kukua, hata kama ataanguka kibiashara, anaweza akaibuka tena kwa sababu tayari amejiweka kwenye mfumo. Mafanikio ni ile hali mtu anakua, na kuifikia hatua ya kuwa kivutio kwa wengine.

Mtu aliyekua kibiashara anaweza akafanya ujasiriamali popote kwa sababu kanuni za mafanikio ni zilezile, mahala popote. Sababu za mtu kufanikiwa ni ile kasi ya ama kuiva (amekua) au kuwa tayari kuwa mfanyabiashara.

Mafanikio yanategemea unajua nini, unafanya nini, una mawazo gani, anaona nini, ni watu gani wanaokuzunguka. Mafanikio ni jambo ambalo liko kisayansi na linaweza kuthibitishwa kisayansi.

Wengi wanakimbia Afrika kwenda Ulaya lakini kila siku tunapishana na Wazungu wanakuja Afrika kwa minajili ya kuwekeza. Hii ni kwa sababu Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji. Waafrika wanakimbilia Ulaya ambako tayari fursa zimeisha.

Kukimbilia Ulaya ni sawa na kwenda eneo ambalo changamoto zimepatiwa ufumbuzi. Huko hakuna tena fursa bali Afrika ndio eneo lenye changamoto tele. Hii ni ishara kuna fursa nyingi ndio maana watu wenye suluhu humiminika Afrika kila mara na kupata fedha nyingi. Waafrika wanapaswa kuwa makini.

Lengo la biashara ni kutatua changamoto zilizopo eneo fulani. Tanzania ina changamoto nyingi hivyo ina nafasi za fursa nyingi za ujasiriamali. Watakaofanikiwa kutatua suluhu hizi ndio watakuwa na mafanikio.

Kutokana na mazingira hayo, hii ndiyo kusema kama kuna mtu anatafuta utajiri anapaswa kufikiria zaidi kuwekeza Afrika na siyo kuangalia uwezekano wa kwenda Ulaya.

Chanzo: mwanachidigital