Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njia rahisi ya kuzalisha uyoga

11894 UYOGA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 22 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua na vumbi.

Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.

Hatua muhimu katika kuotesha uyoga

Mkulima anatakiwa kwanza kutafuta mbegu na baada ya kupata anatakiwa kuwa na mali ghafi kwa ajili ya kuoteshea uyoga na kufanya yafuatayo;

• Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamuliwa.

• Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sentimeta sita au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.

• Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (saa 24).

• Chemsha kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.

• Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.

• Jaza mali ghafi hiyo katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.

Namna ya kupanda

Kuna aina mbili za upandaji wa mbegu za uyoga. Aina ya kwanza mkulima anaweza kuchukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake.

Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.

Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa robo tatu ya mfuko.

Kumbuka: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.

Aina ya pili ni kuchanganya mali ghafi ya kuoteshea (baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1:25 (yaani mbegu moja kwa mali ghafi ya kuoteshea 25).

Kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp), mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni yenye ukubwa wa sm 20 kwa sm 40, ambapo unaweza kujaza kilo moja hadi moja na nusu ya malighafi ya kutoshea. Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.

Mambo ya kuzingatia

Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. Uyoga ni kiumbe hai, hivyo nao unahitaji kupumua.

• Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hifadhi kwenye jokofu na kama huna jokofu, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu.

• Mbegu za uyoga zinaweza kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.

• Unaweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300 kwenye kilo 15 za malighafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.

• Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu isiyo na weupe ni dalili ya kuwa na maambukizo ya vimelea, hivyo haifai kupandwa.

Matunzo ya zao la uyoga

• Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida unaweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza.

• Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14- hadi 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.

• Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba cha mwanga na hewa ya kutosha lakini kisichopigwa jua.

• Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa kwenye meza, chanja ya waya au miti. Lakini pia inaweza kuning’inizwa kwenye kamba. Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko. Maji yawe yaliyochemshwa na kupoa na fanya hivyo mara tatu au zaidi kwa siku.

Tahadhari: Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga. Aina nyingi za uyoga, huanza kutoa vichwa siku mbili hadi tatu baada ya kuwekwa kwenye mwanga.

Uvunaji wa uyoga

Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.

Makala haya ni kwa hisani ya mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org

Chanzo: mwananchi.co.tz