Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nishati jadidifu inavyoweza kulinda mazingira Tanzania

89416 JADDF+PIC Nishati jadidifu inavyoweza kulinda mazingira Tanzania

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makamu mwenyekiti wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), Prosper Magali amesema tani milioni mbili za mkaa zinatumika nchini humo, jambo ambalo linasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Magali ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 20, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu nchini humo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Utu na Mazingira (Hudefo).

Amesema nusu ya matumizi hayo ya mkaa unatumika katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam. Hata hivyo, amesema uelewa wa matumizi ya nishati jadidifu umeongezeka nchini na kwamba jitihada zinahitajika zaidi ili kupunguza matumizi hayo ya mkaa.

"Miti mingi inakatwa kwa ajili ya kuchoma mkaa, huu ni uharibifu mkubwa wa mazingira, tusikubali ukaendelea. Tuhamasishe jamii zetu kutumia nishati nyingine kama vile sola, tungamotaka au nguvu za upepo," amesema Magali.

Amesema nishati jadidifu hapa nchini zinatumika kwa asilimia moja pekee.

Amesema kuna haja ya kuongeza hamasa kwa jamii na wawekezaji ili kutambua umuhimu na fursa zilizopo katika eneo hilo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Sam Kessy amesema wamefanya tathmini ya matumizi ya nishati jadidifu nchini humo na kutengeneza ramani kwa ajili ya kuwaelekeza wawekezaji watakaotaka kuwekeza kwenye umeme wa nguvu za jua au upepo.

Amesema wamebainisha maeneo yenye fursa ya nguvu za upepo kuwa ni Singida na Makambako wakati eneo la Mafia nalo likiwa na fursa ya umeme wa maji kama ilivyo kwa maeneo mengine hapa nchini.

"Tumefanya mapping (bainisha) ya maeneo yote yenye potential (fursa) ya umeme jadidifu, kwa hiyo kama kuna wawekezaji wanataka kuzalisha umeme jadidifu tunawaonyesha maeneo hayo," amesema Kessy.

Kwa upande wake, mdau wa mazingira, Lucas Malebo amesema kilimo kisichofuata utaratibu kinachangia kwa asilimia 24 uharibifu wa mazingira, hivyo ameshauri elimu ya uhifadhi wa mazingira kutolewa kwa wakulima kote nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz