Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Mvutano Latra, Taboa

Mvutano Pic Ni Mvutano Latra, Taboa

Thu, 4 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), ikiruhusu baadhi ya mabasi kuanza safari saa tisa usiku, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimetaka waruhusiwe kuanza safari muda wowote. Ruhusa hiyo ya Latra ilianza kufanya kazi juzi na imelenga mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kigoma na Katavi ambako abiria hulazimika kulala njiani wakati wa safari. Hata hivyo, utaratibu huo bado unapingwa na Taboa, wakitaka mabasi yaruhusiwe kuanza safari muda wowote kwa madai kuwa kitendo cha mamlaka hiyo kuendelea kuyazuia ni kuchelewesha maendeleo. Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano alisema baada ya kupokea ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wameruhusu magari kuanza safari kuanzi saa tisa usiku. “Tulianza kwa majaribio ya safari za saa 11 alfajiri, tumefanikiwa kwa kiasi fulani, sasa tunaangalia ile mikoa ambayo inalazimu magari kulala njiani, kuanza safari saa usiku,” alisema Kahatano wakati akizungumza na waandishi wa habari. Kahatano aliwataka wamiliki wa mabasi yanayofanya safari zake katika mikoa hiyo miwili wanaohitaji kusafiri kwa muda huo kuwasilisha maombi ya vibali Latra ili waruhusiwe. Hata hivyo, akitolea ufafanuzi jana Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo alisema, hakuna sheria inayokataza mabasi kutembea usiku, kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa ile mikoa ambayo wanashindwa kumaliza safari. “Kwa sasa tumetoa maelekezo kwa wale ambao wanaona hawawezi kumaliza safari, tuwape ratiba ya kuanza kama ni saa tisa lakini sharti dereva awe amesajiliwa kwenye mfumo ili linapotokea tatizo tunamuona,” alisema Suluo. Akizungumzia hatua hiyo ya Latra, Naibu Katibu Mkuu wa Taboa, Priscus John alisema bado uamuzi huo hausaidii, jambo la muhimu ni muda wa kuanza safari na sio wa kumaliza. Alibainisha kitendo cha kuzuia mabasi kutembea mchana na usiku, kinarudisha nyuma maendeleo na kuchelewesha kukua kwa uchumi, kwa kuwa wapo watu wanaofanya kazi kwa saa 24. “Yapo magari ya kukodi (special hire) yanafanya kazi kwa saa 24, uhitaji wa usafiri sio wa kwetu ni wa abiria, mtu anaweza kusafiri usiku akaenda sehemu fulani kufunga mzigo na jioni inayofuata akarejea,” alisema John.

Mabalozi wa usalama barabarani

Kutokana na mvutano huo, Ofisa Utawala Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA), Irene Msellem alisema suala hilo liliagizwa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Ndani, akiwa bungeni. Alisema ni kwa nini mamlaka imeshindwa kufanyia kazi na kuruhusu huduma za usafiri kwa masaa 24, hata kwa mikoa ya karibu ya Dar es Salaam - Moshi/Arusha, Dar - Dodoma, ambacho kimekuwa kilio cha miaka kadhaa sasa huku kukiwa na watoa huduma walioomba kufanya hivyo. “Ingawa kwa upande mwingine tunaamini itakuwa hatua nzuri ambayo itatumika kufanya utafiti zaidi wa namna ya kuendelea kuboresha utaratibu wa utoaji leseni na ratiba,” alisema Mselem. Alibainisha RSA, kupitia mabalozi wake kwa ujumla katika mikoa ya Dar, Kigoma, Katavi na mingine, wataendelea kuongeza pia wigo wa kufuatilia, kuibua na kuziripoti changamoto zitakazoibuka. Mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam, Msafiri John alisema, kinachopaswa kufanyika ni kuangalia mazingira yanahitaji nini. “Nafikiri ni wakati wa kuruhusu watu wasafiri saa 24. Kikubwa Serikali iimarishe usalama tu kwani haiwezi kushindwa.” Agizo hilo la Latra limekuja ikiwa ni mwezi mmoja umepita, baada ya kuibuka kwa mjadala bungeni, ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Masaburi (CCM) alihoji ni lini Serikali itatunga sheria kali za kuwadhibiti madereva wazembe. Katika swali la nyongeza mbunge huyo aliitaka Serikali ieleze ni kwa nini iendelee kuzuia mabasi ya abiria kusafiri nyakati za usiku. Kutokana na hoja hiyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alihoji sababu zinazochangia hali hiyo wakati Serikali imejenga na inaendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu nchini. Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alisema magari hayo hayaruhusiwi kusafiri usiku zaidi ya saa sita na kwamba wenye magari ya abiria walishaelekezwa kuweka ratiba zao ili kuendana na muda.

Matukio ya ajali

Kulingana na takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania, ajali za barabarani zimepungua kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2023, ikiripotiwa matukio 229 ikilinganishwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2022 ambapo kulishuhudiwa matukio 588, upungufu huo ni sawa na asilimia 61. Kuhusu vifo vilivyotokea kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023, jumla ya matukio 430 yameshuhudiwa ikilinganishwa na vifo 430 vilivyotokea mwaka jana. Kwa ajali zinazohusisha vifo, vimepungua mwaka huu kwa kipindi cha Januari hadi Machi kutoka matukio 161 kwa mwaka jana hadi matukio 73 kwa mwaka huu, ukiwa ni upungufu wa matukio ya ajali 88 sawa na asilimia 54. Julai 2019 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola alipiga marufuku makamanda wa polisi wa mikoa nchini kuzuia mabasi yanayofanya safari katika ya Jiji la Dar es Salaam na Mikoa ya Kanda ya ziwa kusafiri usiku kwa kisingizio cha kuhofia kuvamiwa na majambazi. Alitoa kauli hiyo katika wa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi wa vijiji vya Namibu na Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara. Alisema mabasi yanayotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam yasizuiwe mkoani Morogoro.

Chanzo: mwanachidigital