Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngozi za paka, mbwa kutengeneza mapambo?

Ef5895a0ba193ed49f3424e0fa85429a.jpeg Ngozi za paka, mbwa kutengeneza mapambo?

Thu, 18 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imezitaka taasisi za utafiti nchini kufanya utafiti zaidi katika maeneo ya wanyama wafugwao wakiwamo paka, mbwa, mbuzi na kondoo ili mazao ya wanyama hao yote yatumike kama malighafi kutengeneza bidhaa na mapambo kupitia ngozi, meno na viungo vingine.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Profesa Elisante ole Gabriel wakati akizungumza kwenye kipindi cha Morning Express kinachurushwa hewani na Kituo cha Redio cha Uhai Fm kinachomilikiwa na Kampuni ya Azam Media.

Akizungumzia hilo, Profesa Gabriel alisema taasisi zilizopo nchini za utafiti ikiwemo Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), zimekuwa zikifanya kazi zao vizuri na hivi sasa kuna tafiti zinaendelea katika ngozi za wanyama ili kuhakikisha hakuna malighafi inayotupwa.

“Lengo letu tufike mahali katika mifugo yetu hakuna kitakachochupwa, tunataka wanyama wafugwao kama paka na mbwa nao tafiti zifanywe ili tuone ngozi zao zinatumika kutengeneza bidhaa na mapambo,” alisema.

Katika hilo, aliwataka TIRDO pia kufanya utafiti kwenye viungo vya wanyama wafugwao mfano meno ya mbuzi, kondoo na wanyama kama hao ili viungo hivyo visitupwe bali vitengeneze mapambo na bidhaa nyingine.

“Sasa kwenye hili naomba wale wafugao paka na mbwa wasiwe na wasiwasi au woga kwamba wanyama wao watauawa ili kuchunwa ngozi, hapana! Tafiti lazima zifanywe na sheria za wanyama zitalindwa ili kama ngozi zao zitakuwa na soko basi ni lazima pia tuwafundishe wananchi jinsi ya kuwafuga kibiashara wanyama hao kwa ajili ya kuja kuwauza kwa ajili ya kuvuna ngozi,” alisema.

Akitoa takwimu alisema hivi sasa Tanzania inashika nafasi ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo.

Mifugo hiyo ni ng'ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.65, punda 653,800, nguruwe milioni mbili, kuku milioni 83, mbwa milioni 3.5 na paka milioni tatu.

Alisema Tanzania kwa sasa viwanda vilivyopo ni tisa vinavyosindika mazao ya ngozi na kwamba kati ya hivyo vinavyofanya kazi ni vitano na mahitaji ya ngozi ni vipande vikubwa milioni 2.5.

Profesa Gabriel alifafanua kuwa pamoja na mahitaji hayo kwa sasa uwezo wa viwanda nchini kusindika ngozi ni hadi vipande milioni 4.7 kwa vipande vikubwa na kwa vipande vidogo ni hadi milioni 8.11.

Alisema kwa upande wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini, viatu vya ngozi ndio vinaongoza ambavyo uzalishaji wake ni jozi milioni 1.2 na mwaka jana vilizalishwa jozi milioni 38 na mahitaji ya mwaka huu ni kuzalisha jozi milioni 54.

“Utaona fursa za bidhaa za ngozi zipo kinachotakiwa ni watanzania kubadilisha mtazamo na kupenda bidhaa,” alisema na kuongeza viwanda vya ngozi nchini vinafanya kazi na kuvitaka viongeze uwezo wao wa kusindika ngozi ili malighafi hiyo ipatikane kwa urahisi.

Alisema anafahamu changamoto za viwanda hivyo ni fursa za masoko ya malighafi hizo na kusema viwanda vinazalisha kutokana na soko lilivyo na kuhimiza pia wananchi na wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya soko la ngozi ili wazitumie kutengeneza bidhaa bora.

Chanzo: www.habarileo.co.tz