Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ng'ombe 25,000 wafa kwa ukame

Ngombe Pic 1 Data Ng'ombe 25,000 wafa kwa ukame

Sun, 13 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya ng’ombe 25,000 wamekufa katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kutokana na ukosefu wa maji na malisho hali iliyokumba baadhi ya maeneo hapa nchini.

Akizungumza Februari 12, 2022 wakati wa makabidhiano ya bwawa la maji lililochimbwa na Kampuni ya Uwindaji ya Sunset Safaris, Mkuu wa wilaya hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Mbaraka Batenga amesema hali hiyo imechangiwa na upungufu wa vyanzo vya kutosha vya maji.

“Hatuna vyanzo vya kutosha vya maji kwa ajili ya mifugo kwa takwimu tulizonazo kwa kipindi tulichopigwa na ukame tumepoteza mifugo mingi ambapo ngo’mbe zaidi ya 25,000, wamekufa sababu kubwa ni ukosefu wa majani na maji,”

Amesema kuchimbwa kwa bwawa hilo katika Kijiji cha Katikati Kata ya Makame, litasaidia kupunguza vifo vya mifugo pamoja na wanyamapori ambao wamekuwa wakivamia vijiji na kuharibu mazao huku wengine wakitumbukia katika visima vya maji.

“Kipindi cha ukame hii ni changamoto kubwa kwa kipndi kilichopita tumepata changamoto ya ukame iliyokuwa inalazimu wanyama wanatoka porini wanaingia kwenye vijiji vya Katikati,Ngabolo  na Ndedo na kila mara tulikuwa tukienda kuwaokoa baadhi ya wanyama wanaodumbukia katika visima vya asili vya wananchi,”

“Tulikaa na mwekezaji ambaye amewekeza katika kitalu cha Makame WMA, nichukue nafasi hii kushukuru walikubali kuchimba bwawa hili hapa ambalo litakuwa ufumbuzi wa tatizo la maji kwa kiasi kikubwa katika eneo hili,”amesema Mkuu huyo

Advertisement Mkurugenzi wa Kampuni ya uwindaji ya Sunset Safaris, Saleh Al Amry (katikati) akimweleza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga juu ya ujenzi wa bwawa la maji katika Kijiji cha Katikati Kata ya Makame. Picha na Janeth Mushi

Awali akitoa taarifa ya bwawa hilo Mkurugenzi Sunset Safaris, Saleh Al Amry amesema bwawa hilo walilolichimba kwa zaidi ya miezi miwili hadi kukamilika kwake litaghamu zaidi ya Sh 600 milioni.

Alisema lengo la kuchimba bwawa hilo na kusaidia jamii ya eneo hilo hasa akina mama waliokuwa wakiteseka kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pamoja na mifugo na kuwa litasaidia wanyamapori pia.

“Sisi tumeamua kufanya hili jambo kwa sababu tunamiliki hiki kitalu,hili bwawa liko eneo la kitalu chetu tumeona adha wanayopata wananchi na sisi tumeamua tuchangie msaada huu kama kurudisha sehemu ya faida kwa jamii,”amesema

“Hili bwawa lina upana wa mita 300 na urefu wa kilomita moja na chini linaenda mita 10, mifugo ya wananchi ilikuwa ikikosa maji inaingia pori tengefu la Mkugunero, ikiingia inakamatwa,”

Mkurugenzi huyo amesema baada ya kukamilika kwa bwawa hilo na mvua kupungua,wana mpango wa kuchimba bwawa lingine nyuma ambalo litatumika kuchuja matope ili maji yanayoingia hapo yawe safi zaidi kwa ajili ya matumizi.

“Hili bwana baada ya mvua kuisha watu wataweza kutumia maji haya kwa amtumizi ya nyumbani pia kwani hapa kijijini wana kisima ila cha maji yenye chumvi,kipindi tumekuja tulikuta wanawake wanahangaika kuchimba kwenye tope kupata maji ya kunywa,"amesema

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa kijiji hicho,Nongoyoyo Lengohok amesema wananchi 2,054 wa kijiji hicho watanufaika na uwepo wa bwawa hilo ambapo awali miaka ya nyuma kabla halijachimbwa lilikuwa likikauka kipindi cha ukame.

“Tunamshukuru mwekezaji kwani tunatarajia malalamiko ya maji yataisha hasa ng’ombe hawatahama kwenda vijiji vya nje kutafuta maji,”amesema

“Awali kabla ya bwawa tulikuwa tunateseka tulikuwa tunategemea vijiji vya jirani hadi Wilaya ya Chemba na wakati mwingine ikawa vurugu zinatokea kila mara,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wazee wa mila maarufu kama Laigwanan wilayani Kiteto,Ngaiyeni Bakari amesema wanawake walikuwa wakiteseka kwenda na punda umbali mrefu kutafuta maji na kuwa wakati mwingine walikuwa wakitumia siku nzima kutafuta huduma hiyo muhimu.

“Bwawa hili litasaidia kwani bila maji huwezi kuishi, akina mama walikuwa wanaamka alfajiri saa 10, wanapika chakula kabisa na kwenda kufuata maji umbali mrefu,wakati mwingine anaweza kutumia siku nzima kupata huduma hiyo,”amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live