Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Neema kwa wachimbaji wadogo wa madini yaja

Wachimbaji Mdogo Baadhi ya wanufaika watarajiwa wa madini

Sat, 16 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania imefanikiwa kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi nne (4) Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (Organisation of African, Caribbean and Pacific States-OACPS) zitakazonufaika na Program ya ufadhili wa umoja wa Ulaya wenye jumla ya Euro milioni 11.1 sawa na takriban shilingi bilioni 30 kwenye sekta ya madini.

Program hii inayoitwa (OACPS-EU Development Mineral Programme) inalenga kuboresha mazingira ya uchimbaji madini na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo hususan vijana na wanawake katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022 – 2024.

Uamuzi huu umetangazwa na Secretarieti ya OACPS ambayo makao makuu yake yako Brussels nchini Ubelgiji. Mbali na Tanzania, nchi zingine 3 za Jumuiya ya Afrika, Carribean na Pacific zilizofanikiwa kuchaguliwa kwenye program hii ya awamu ya pili ni Burkinafaso, Jamhuri ya Kongo na Suriname.

Utekelezaji wa program hii utachochea sekta ya madini katika nchi za OACPS kutoa mchango stahiki katika kuongeza mnyororo wa thamani ya madini, uzalishaji wa nafasi za ajira na ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Upatikanaji wa nchi za kunufaika na awamu ya pili ya programu hii uliyoanza mchakato wake mwezi Agosti mwaka jana, ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na idadi kubwa ya nchi zilizojitokeza kuomba zijumuishwe kwenye program hiyo. Jumuiya ya OACPS ina jumla ya nchi 79, hivyo kuchaguliwa kwa Tanzania kunufaika na programu hii ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa ushawishi wa Tanzania ndani ya Jumuiya ya OACPS na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha ushirikiano na Jumuiya hiyo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na ubalozi wa Tanzania ulioko Brussels, Ubelgiji.

Utekelezwaji wa programu hii utafanywa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Wizara ya Madini chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

Ni matarajio yetu kuwa, ujumuishwaji wa Tanzania katika utekelezaji wa programu hii, pamoja na kusaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini, pia itawaongezea maarifa na ujuzi wachimbaji wadogo hususan vijana na wanawake. Serikali kupitia Wizara ya Madini inajiandaa ipasavyo kuanza utekelezaji wa programu na tunatoa rai kwa wadau wa sekta ya madini hasa wachimbaji wadogo kuchangamkia ipasavyo fursa zitakazotokana na program hii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live