Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndumbaro kuja na mwarobaini mnada vitalu vya uwindaji

Vitalu Uwindaji.jpeg Ndumbaro kuja na mwarobaini mnada vitalu vya uwindaji

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro atatoa hatima ya utata juu ya vitalu vilivyoingia dosari wakati wa mnada wa sita wa kielektroniki wa vitalu vya utalii wa uwindaji.

Akizungumza mjini hapa jana baada ya kusikiliza malalamiko juu ya vitalu hivyo, Dk Ndumbaro alisema Februari 16 atatoa majibu kama vitatu hivyo apewe mshindi au mnada urudiwe.

Wakati akisikiliza malalamiko hayo, Ofisa Mwendeshaji wa Kampuni ya Trophy Belt, Emmanuel Nyasingo ambaye kampuni yake ilishinda vitalu vinne katika mnada huo aliwasilisha nyaraka za kuonyesha uwezo wake.

Awali, Ofisa wa Tawa, Emmanuel Musamba alisema baada ya kampuni hiyo kushinda na kufanyiwa uhakiki, walibaini kutokuwa na nyaraka zinazotakiwa kisheria ikiwamo bondi kutoka benki na mpango wa biashara.

Kwa upande wa kitalu cha Lake Natron South, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilombero North Safari, Akram Aziz alipinga ushindi katika kitalu hicho kwa madai aliyeshinda hakua amesajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), muda wa mnada uliongezwa na kuwa mfumo ulikuwa unamkata dakika 30 za mwisho.

Akitoa ufafanuzi, Musamba alisema mfumo unaruhusu kampuni kuwapa watumiaji wengine walio katika kampuni fursa ya kuingia kwenye mfumo na kuwa mnada ulifungwa Januari 13 saa 5:59:59 na mshindi alishinda kwa kutenga Dola za Marekani 192,000.

Kwa upande wa Kitalu cha Bulko, Mkurugenzi wa Kampuni Bushman Hunting Safari Ltd, Talala Abood aliomba radhi kutokana na makosa ya kuandika kiwango kikubwa cha Dola za Marekani 400,000 badala ya dola 40,000, hali ambayo ilifanya wawekezaji wengine kushindwa kushiriki mnada.

Dk Ndumbaro aliwaagiza wataalamu wa Tehama wa Tawa kuboresha mfumo wa mnada ili kutoa fursa ya wawekezaji kutumia dakika za mwisho kushiriki kwenye mnada huo.

"Kwa maelezo yaliyotolewa hapa, inaonesha wawekezaji wengi wanapenda kushiriki mnada dakika za mwisho jambo ambalo linasababisha foleni ambayo inawafanya wengine kukosa fursa, sasa mje na suluhu ya kuondoa changamoto hiyo ili wakiwa wanapambana wapambane mpaka dakika za mwisho," alisema.

Dk Ndumbaro pia aliwasihi wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuacha kupigana vita na vijembe, kwani hali hiyo inarudisha nyuma sekta ya utalii na kueleza kuwa wizara itasimamia sheria, kanuni na taratibu katika kuendesha sekta hiyo.

Naibu Waziri, Mary Masanja aliwataka wawekezaji waliokosa fursa hiyo kusubiri mnada wa saba ambao utafanyika muda wowote ndani ya mwezi huu.

Alisema serikali ina mkakati wa kufungua maeneo mengine ya uwekezaji huku akiwasihi kutumia Mpango wa Uwekezaji Mahiri (Swica) ambao unatoa fursa ya kuwekeza kwa muda mrefu

Chanzo: www.tanzaniaweb.live