Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndumbaro ataka mkutano kujadili ongezeko la watalii

D9f7a84f9d488cc84c5748f08eccbadf Ndumbaro ataka mkutano kujadili ongezeko la watalii

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zinahitajika kukaa pamoja na watoa huduma wakubwa wa ndege na mashirika ya kimataifa ya ndege kuona namna bora ya kuongeza idadi ya watalii nchini.

Lengo la kuketi pamoja na kuzungumzia changamoto na kuziondoa ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alisema hayo wakati akifunga mkutano wa siku nne uliomalizika juzi mjini Morogoro kwa wadau wa utalii uliojadili namna ya kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini.

Wadau walioshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja wakala wa uwindaji wa kitalii, wasafirishaji watalii, waongozaji watalii na wakala wa safari za ndege, watoa huduma za malazi, wadau wa usafirishaji wa anga na meli.

Alisema umefika wakati wizara yake na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kukaa na watoa huduma wakubwa wa ndege kama Ethiopian Airline, KLM, Swiss Air, Fly Dubai, Qatar Airways waweze kufikia malengo waliyojiwekea ya kuongeza idadi ya watalii nchini.

Waziri hiyo alisema utalii una mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa na sekta hiyo inachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa ambapo ukichanganya na Sekta ya Misitu inafikisha asilimia 22.

Hata hivyo alikipongeza Chama cha Wamiliki wa Ndege Tanzania ( TAOA) kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika uchumi wa nchi hususani kwenye sekta ya utalii .

“Niwaombe wenzetu wa Uchukuzi tuuangalie Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa jicho la kipekee, sisi watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii tunajaribu kutafakari tunawezaje kuifanya KIA kuwa ni “Special Tourists Free Zone,”alisema.

Waziri huyo pia aliwataka wataalamu wa wizara yake watafakari suala la Leseni ya Waendesha Huduma za Utalii (TALA) katika sekta ya Maliasili na Utalii, ya kwamba kuna vitu lazima viangaliwe kwa kuwa vinaathiri uchumi, watoa huduma wasiadhibiwe kwa kuwaongezea tozo zisizokuwa za lazima.

Dk Ndumbaro alisema kutokana na Rais John Magufuli kutofunga mipaka ya nchi mwaka 2020 kutokana na ugonjwa wa Covid-19, sekta ya utalii ilipata watalii zaidi ya 600,000.

“Huu ni muda wa kuwapa taarifa wale waliojifungia, tuwape taarifa kwamba sisi tuna Serengeti, tuna Hifadhi ya Mikumi, Nyerere, Tarangire na nyingine nyingi,” alibainisha.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi alisema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020- 2025 imeipa wizara jukumu la kuongeza zaidi mapato hadi kufikia Sh bilioni sita na idadi ya watalii hadi kufikia milioni tano kufikia mwaka 2025.

“Haya ni majukumu makubwa ambayo Wizara inahitaji kushirikiana na wadau ili kutimiza lengo hili, tuna imani kwa pamoja tutaweza kutekeleza na kutimiza lengo lililowekwa” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz