JANA gazeti hili liliongozwa na habari kuu iliyobeba kichwa cha habari, “Tanzania yatajwa nchi salama zaidi duniani,” ikirejea taarifa iliyotolewa na Baraza la Wasafi ri na Utalii Duniani (WTTC).
Baraza hilo limeipa Tanzania nembo ya Mhuri wa Usalama wa Wasafiri ambayo imetokana na nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi salama zaidi duniani, hivyo stempu iliyotolewa itabandikwa katika kila tangazo linalohusu utalii wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, watalii wengi kabla ya kufanya uamuzi wa kutembelea nchi yoyote huwa wanataka kujihakikishia usalama wa nchi husika kuanzia ulinzi, huduma za vyakula, malazi na usafiri, hivyo stempu hiyo itawapa uhakika wa kupata huduma hizo.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada zilizofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli, kuhamasisha maendeleo ya sekta ya utalii, na kutoa hamasa kwa wadau kuboresha mazingira ya utalii hadi kufikia hatua ya kukubalika kimataifa.
“Hakika hii ni hatua kubwa na yenye mafanikio kwa nchi yetu, hii stempu inatuweka katika mazingira shindani zaidi ya utalii na nchi nyingine, kikubwa ni kuendelea kuitunza heshima hii kwa kuhakikisha kuwa zile sababu za kupatiwa stempu hii zinazidi kuimarika,” alisema Dk Kigwangalla.
Hakika hii ni hatua kubwa sana katika suala la utalii nchini, ikizingatiwa kwamba Tanzania imekuwa ikitegemea mapato ya utalii katika kukuza Pato la Taifa. Kwa mujibu wa takwimu, mwaka jana utalii ulichangia asilimia 17 ya Pato ya Taifa, ajira za moja kwa moja 600,000, ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya milioni 1.2 na kuchangia mapato ya fedha za kigeni kwa asilimia 25.
Kwa kuangalia takwimu hizo, ni hakika mchango wa sekta ya utalii kwa Tanzania ni mkubwa, na kama alivyoeleza Dk Kigwangalla, kumekuwa na jitihada kubwa za serikali katika kuhamasisha maendeleo ya sekta hiyo na haishangazi kuona matunda yake yanazidi kuongezeka siku hadi siku.
Ndio maana sisi tumefarijika na kutolewa kwa stempu hiyo muhimu katika sekta ya utalii, ikionesha kuwa Tanzania ni nchi salama zaidi duniani, na hivyo ni habari njema katika kuvutia watalii na wageni wengine kwa ujumla kuja nchini.
Tanzania kwa miaka mingi imekuwa kisiwa cha amani duniani, hivyo kutajwa na kutolewa kwa stempu hiyo ni mwendelezo wa kuthibitisha utulivu wa Tanzania, jambo ambalo tunawathibitishia wageni na watalii kwa ujumla kuwa Tanzania ni mahali salama kwa kuja na wanakaribishwa.
Kutolewa kwa stempu hiyo ni mafanikio makubwa kwa nchi, na kwa msingi huo tunawaomba Watanzania waendelee kudumisha amani na utulivu ili Tanzania inufaike, siyo tu kwa kuingiza watalii wengi, bali pia kuja kwa wageni wengine wengi wakiwamo wawekezaji katika sekta nyingine za uchumi