Mtendaji Mkuu wa kampuni inayobeba bendera ya Tanzania (Air Tanzania Company Limited - ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL kupitia mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ambao ulianza mwaka wa fedha 2022-2023, inategemea kupokea ndege nyingine mpya ya masafa marefu mwezi Aprili mwaka huu.
Amesema hayo leo Machi 26, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina Boeing 737- 9MAX iliyotoka Seattle, Marekani hadi Tanzania.
Aidha Matindi amesema kupitia mpango mkakati huo ATCL inategemea kuwa na ndege 20, lakini mpaka sasa ATCL ina jumla ya ndege 14 zilizonunuliwa na serikali pamoja na ndege ndogo aina ya Dash 8-Q300 ambayo ilikuwepo kabla ya ufufuaji wa shirika, yaani kabla ya kuanza kwa mwaka 2016 na hivyo kuwa na jumla ya ndege 15.