Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndayimishiye aeleza TPA inavyorahisisha biashara Burundi

Tpa Pc Data Ndayimishiye aeleza TPA inavyorahisisha biashara Burundi

Sun, 24 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Rais wa Burundi, Evariste Ndayimishiye amesema utendaji kazi wenye ufanisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), umerahisisha ufanyaji wa biashara nchini kwake.

Rais Ndayimishiye ambaye amekuwa nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, ameyasema hayo leo Jumapili Oktoba 24, 2021 wakati alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea shughuli mbalimbali na kuzungumza na watendaji.

Kiongozi huyo ambaye amechukua mikoba ya marehemu Pierre Nkurunzinza, alianza ziara yake jijini Dodoma, Zanzibar kisha Dar es Salaam. Pia, amemshukuru Rais Samia na Watanzania kwa ujumla kwa kumpa mapokezi makubwa na mazuri.

Amesema TPA imekuwa na utendaji wenye ufanisi na ambao umesaidia kurahisisha biashara, akitolea mfano uamuzi wa mamlaka hiyo wa kufungua ofisi zake jijini Bunjumbura, Burundi hatua iliyoleta urahisi kwa wafanyabiashara wake kusafirisha bidhaa maeneo mbalimbali.

“Nawashukuru sana kwa kunikubalia kuona bandari kwa sababu miaka iliyopita nilikuwa napita pembeni pembeni, nikiona kwa macho. Nawaomba msichoke na huduma zenu kwa wafanyabiashara wa Burundi,” amesema Rais Ndayimishiye.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi amesema Bandari ya Dar es Salaam ina magati 12 zenye urefu wa mita 2,482 na uwezo wa kuegesha meli 11 kwa wakati mmoja zenye urefu wa mita 200 hadi 260.

“Gati tulizonazo hapa zina uwezo wa kuhudumia shehena za magari, pia tuna eneo la kuhudumia makasha, mizigo mchanganyiko, nafaka na mafuta. Mheshimiwa Rais Ndayishimiye leo umekuja na baraka katika gati zilizopo kuna meli tisa zinazohudumiwa kwa wakati huu.

“Nje ambako meli zinaweka nanga zipo 11, jumla zinakua meli 20 zilizopo Tanzania na ndani ya saa 24 zimeshatoka meli mbili. Jana kulikuwa na meli ya magari 1,561 kati haya 960 yalikuwa yakienda nchi za nje ambapo 44 yalikuwa ya Burundi,” amesema Hamissi.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema wizara yake imefarijika kuona uhusiano wa kibiashara kati ya Burundi na Tanzania umeimarika kila wakati na kwamba, jitihada hizo zitaendelewa.

Chanzo: mwananchidigital