Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi ina mchele wa kutosha

Be1bbac48491344a3c03c71575565238 Nchi ina mchele wa kutosha

Mon, 3 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KILIMO cha mpunga nchini kimeongezeka katika kipindi cha miaka minne sasa, hivyo kuifanya nchi kuwa na mchele wa kutosha na kwamba katika kipindi hicho hakuna kibali cha kuagiza mchele kutoka nje kilichotolewa.

Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi na Udhibiti Ubora wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Tanzania (NIRC), Daniel Manase katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ya 27 maarufu Nanenane, yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Alisema sekta ya kilimo kwa ujumla inachangia asilimia 58 ya pato la taifa na kwamba kilimo cha umwagiliaji kimeongeza mchango katika pato hilo, ambapo asilimia 24 kati ya hiyo 58 inatokana na kilimo cha umwagiliaji.

Alisema kwa sasa nchi inajitosheleza kwa mchele, kwani kwa miaka minne sasa wameshuhudia mavuno yakiongezeka kutoka tani milioni 1.6 za mchele mwaka 2014/15 hadi kufika tani milioni mbili mwaka jana.

"Utaona juhudi zimefanywa za kuongeza uzalishaji wa chakula nchini kwa kuongeza eneo la umwagiliaji na sasa uzalishaji wa mpunga tunaopata mchele umekuwa mzuri, wakulima wengi wanatumia kilimo cha umwagiliaji na tunapata mavuno mengi, hatuna tena uhaba wa mchele, tunajitosheleza,"alisema Manase.

Kwa msimu wa mwaka 2020/21, wanategemea kwenye kilimo cha mpunga kuzalisha tani milioni 2.9 za mchele na hiyo kuifanya nchi kuendelea kuwa na kiasi cha kutosha cha bidhaa hiyo, hivyo fedha zilizokuwa awali zinatumika kuagiza mchele nje ya nchi sasa zitatumika kuendeleza miundombinu mingine.

Manase alisema NIRC hivi sasa imejipanga kuendeleza skimu za umwagiliaji na kutoa mafunzo kwa wakulima ikiwemo wakulima wa pamba, vitunguu, mahindi na mazao ya mbogamboga ili kulima kwa tija na kupata mavuno mengi.

Akitoa mfano, alisema kuwa wataalamu wa NIRC waliopo nchi mzima kwenye halmashauri mbalimbali, wanaendelea kuwafikia wakulima kupitia vikundi vyao na kuwapa mafunzo ya jinsi ya kutumia kulimo cha umwagiliaji na kupata mavuno bora hata kwenye eneo dogo.

Manase alisema kuwa kwa sasa katika hekta moja ya vitunguu inayolimwa kwa kutumia skimu ya umwagiliaji inatoa mavuno tani 26 wakati awali kwenye eneo hilo kwa kutumia kilimo cha mvua mkulima alikuwa akipata tani 13 tu, kama mvua zikinyesha vizuri.

Ofisa Kilimo wa NIRC kutoka Mwanza, Peter Sarwat akizungumzia kilimo cha kitalu nyumba na umwagiliaji kwa njia ya matone, alisema kimesaidia wakulima wengi kupata mazao mengi na kupunguza gharama ikiwemo kulima kwenye eneo dogo na kupata mazao mengi yaliyo bora.

Sarwat aliwataka wananchi na wakulima kupitia maonesho hayo, kutembelea banda hilo kupata elimu na kujua afisa kilimo aliye kwenye eneo lake ambaye atamsaidia kufanikisha ndoto zake za kubadilisha aina ya kilimo kuwa cha tija na faida.

Chanzo: habarileo.co.tz