Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Nazi bora zitapunguza uhaba wa mafuta ya kula’

60a4f75abad6edcad87eec312ba76eeb ‘Nazi bora zitapunguza uhaba wa mafuta ya kula’

Tue, 1 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MADINA Ismail, mkazi wa Dar es Salaam anasema yeye na familia yake hupenda kula chakula kilichoungwa ya nazi.

“Tarehe hizi nazi zinepanda bei kidogo sokoni ingawa wakati mwingine ninanunua nazi za paketi madukani. Chakula cha nazi ninakifurahia sana,” anasema.

Ingawa hajui kama nazi haina lehemu nyingi (cholesterol) inayochangia matatizo ya kiafya kulinganisha na aina nyingine za mafuta, Madina anasema chakula kilichoungwa nazi kina ladha nzuri kulinganisha na kuungia mafuta mengine.

Anasema yeye pia hupendelea kutumia mafuta ya nazi kujipaka mwilini baada ya kusikia ni mafuta bora kulinganisha na aina nyingine za mafuta.

Kwa upande wake, Tatu Juma, mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam, anasema awali hakujua kama mafuta ya nazi yaliyokamuliwa bila kuchemshwa yanaondoa vipele, mapunye na magonjwa ya ngozi.

Anasema mtoto wake alipoungua mapunye, akashauriwa kutumia mafuta ya nazi ambayo hayajapikwa kumpaka mwanawe na alipoanza tiba hiyo ikampa matokeo chanya.

Mbali na kupikia na kujipaka, sabuni pia zinaweza kutengenezwa kwa mafuta ya nazi na hivyo kuwa nzuri kwa kuogea kulinganisha na sabuni zinatengenezwa kwa kemikali.

Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mikocheni jijini Dar es Salaam, Dk Zuberi Bira, anasema nazi ni zao muhimu linaloweza kusaidia kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.

Mahitaji ya mafuta ya kula yanatajwa kuwa tani takribani 770,000 kwa mwaka lakini mafuta yanayozalishwa ni tani 205,000 na hivyo kusababisha nchi kutumia pesa nyingi za kigeni kuagiza nje kiasi cha tani 365,000 za mafuta.

Kutokana na umuhimu huo Bira anaishauri serikali kulifanya zao la nazi kuwa la kimkakati ili liweze kuchangia katika kumaliza upungufu wa mafuta nchini.

Hii pia imekuwa ikidhihirishwa na ukweli kamba Kitengo cha Mafuta cha Kurasini (KOJ) Dar es Salaam cha Mamlaka ya Bandari Tanzania, kimekuwa kikipoka mafuta mngi ya kupikia kutoka nje.

Msimamizi wa KOJ, Kapten Sixtus Karia aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema kwamba hajawahi kuona mafuta ya kula kutoka nchini yakisafirishwa kwenda nje zaidi ya sisi kupokea idadi kubwa ya mafuta ya kula kutoka nje.

Ni katika muktadha huo TARI imekuwa ikifanya utafiti ili kupata mbegu bora za mazao mbalimbali yanayozalisha mafuta ikiwemo nazi.

Bira anafafanua kwamba mbegu wanazotafiti ni zile zinazoweza kuhimili ukame, magonjwa na wadudu ili kuongeza uzalishaji na tija kwa taifa.

Meneja huyo anasema nazi zinazopatikana kwa mwaka nchini ni milioni 800 huku ikikadiriwa kwamba nazi 15 hadi 20 hutoa lita moja ya mafuta.

Endapo nazi zote milioni 800 zitakamuliwa zitatoa tani 58,000 za mafuta na kuchangia kwenye zile tani 365 zinazolazimika kuagizwa nje ya nchi.

Anasema mkulima akitumia njia bora za kilimo kwa zao hilo anaweza kupata hadi nazi 100 kwa mnazi mmoja kwa mwaka badala ya kati ya nazi 15 hadi 20.

Ni kwa mantiki hiyo Meneja Bira anashauri wananchi kutumia mbegu bora aina ya East African Tall (EAT) ambayo inavumilia ukame pamoja na ukinzani dhidi ya magonjwa.

Anasema soko la nazi nchini Tanzania ni zuri lakini pia nazi zina soko la uhakika katika nchi jirani za Zambia, Burundi, Comoro na Kenya.

Akielezea changamoto kubwa iliyopo kwa sasa anasema ni uwepo wa minazi mingi mizee iliyokaa zaidi ya 100 na hivyo uzalishaji wake kuwa mdogo.

Anasema hata wanaopanda minazi sasa wanatumia mbegu zisizo na tija kwani hazitoi mazao mengi na ni rahisi kushambuliwa na wadudu.

“Kama unataka upande mazao mengine ya muda kwenye shamba la mnazi unaweza kupanda kwa nafasi ya mita 10 kwa mita 15. Ambayo hiyo hekta moja moja itakupatia minazi 67. Lakini ukipanda mita 10 kwa 10 utapata minazi 100 kwa hekta,” anasema.

Anasema kutokana na faida ya minazi, anahimiza wakazi wa maeneo ambayo nazi hustawi kwa wingi kama mikoa iliyopo pwani ya Bahari ya Hindi, Kando Kando ya Ziwa Victoria, Mbeya – Kyela, Morogoro na Visiwa vya Zanzibar kuchangamkia kilimo cha zao hilo.

Anasema wakitumia njia bora za kilimo wanaweza kupata nazi mpaka 100 kwa mnazi mmoja kwa mwaka na hususani kwa mbegu zinazohimili visumbufu ambavyo ni pamoja na ugonjwa wa kunyong’onyea kwa minazi ambao hauna tiba.

Anasema mbegu bora zilizotafitiwa zipo za aina nne ambazo ni EAT Boza, EAT Mwambani, EAT LBS na EAT VUO.

“Zote zimefanyiwa uchunguzi wa muda mrefu katika eneo la Chambezi, Bagamoyo mkoani Pwani,” anasema.

Anataja kisumbufu kingine kuwa ni ukame lakini aina hiyo ya minazi inastahimili ukame pamoja na wadudu waharibifu.

Anasema kiafya, mafuta ya nazi yanayotumika kwa njia mbalimbali ikiwemo kupikia, kujipaka hata kunywa yanasaidia kupunguza matatizo ya maradhi mbalimbali hususani mafuta yaliyokamuliwa kwa njia za kiasili bila ya kuweka kemikali au kuchemshwa.

Anasema mbali na mafuta ya kula na kujipaka miti ya minazi pia hutoa samani mbalimbali ikiwemo mapambo.

Kwa kuwa minazi mingi imezeeka, inapaswa kukatwa na kutengenezwa samani na wahusika kupanda miti inayotakana na mbegu za bora.

Hata hivyo, anasema pamoja na jitihada za uhamasishaji na uzalishaji wa mbegu bora za kutosha bado wakulima wengi hawafuati kanuni bora za kilimo cha minazi.

Changamoto nyingine anasema ni upanukaji wa makazi ya watu, hususani maeneo ya Pwani na kusababisha minazi mingi kukatwa ili kupisha makazi ya watu.

Bira anasema mikakati ya TARI kupitia kituo cha Mikocheni ni kuhakikisha elimu inawafikia wakulima na wadau mbalimbali kuhusu kilimo bora cha minazi lakini pia utumiaji wa mbegu bora za minazi.

Kwa kuliona hilo kituo hicho cha Mikocheni kimeanza mkakati wa kuwafikishia wakulima mbegu na miche ya minazi ambayo ni bora katika wilaya ya Pangani kwa kuwa wanazalisha nazi nyingi ingawa minazi mingi ni mizee.

Mkakati mwingine kwa siku za baadaye anasema ni kupeleka miche badala ya mbegu kwa kuanzisha vitalu ambavyo kwa sasa hatua hiyo ina changamoto ya ufuatiliaji na umwagiliaji hasa wakati ambao sio kipindi cha mvua.

Kuhusu usambazaji wa mbegu Bagamoyo, Bira anasema tayari wana kitalu chenye miche takribani 6000.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo anasema serikali itaokoa kiasi cha Sh bilioni 400 mpaka 675 kwa mwaka za mahitaji ya mafuta ya kula nchini, yanayoagizwa kutoka nje ya nchi baada ya kuwepo kwa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya alizeti na michikichi nchini.

Anasema uagizwaji huo mkubwa wa mafuta kutoka nje unafanyika wakati nchi ikiwa na uwezo wa kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya mafuta ya kula, hivyo taasisi hiyo inatafiti mbegu bora zenye tija pamoja na kuwafundisha wakulima teknolojia bora za kilimo ili kulima kilimo chenye tija na kuongeza uzalishaji.

“Kituo cha Mikocheni kina mazao mawili inayoyashughulikia ambao ni zao la minazi na eneo la pili ni tafiti za bayoteknolojia,” anasema.

Anasema taasisi hiyo inahakikisha teknolojia mbalimbali ambazo zimegunduliwa zinawafikia wakulima kwa kuwa itakuwa haina maana zisipokuwa na mchango wowote kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TARI, Dk Yohana Budeba anasema kilimo ni uti wa mgongo hapa nchini hivyo anaipongeza serikali kwa kuanzisha TARI kwani inaendelea kuleta mageuzi ya kilimo nchini kwa kujibu changamoto za wakulima kupitia tafiti zinazofanywa.

Chanzo: habarileo.co.tz