Nauli mpya za mabasi ya mwendo wa haraka zitaanza kutumika kuanzia Jumatatu Januari 16, 2023 lakini nauli ya wanafunzi itabaki ileile ya Sh200.
Hatua hiyo inakuja baada ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuridhia maombi yaliyowasilishwa katika mkutano uliofanyika Januari 3, 2023 kati ya mkurugenzi wa Latra, Habibu Suluo na waandishi wa habari alisema nauli hizo zitanza kutumika baada ya siku 14 zijazo.
Katika mkutano huo mbali ya kutangaza nauli za mabasi hayo, pia alitangaza kuridhia nauli mpya za teksi mtandao.
Leo Jumamosi Januari 14, 2023 kupitia ukurasa wao katika mtandao wa kijamii wa Instagram, Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), ambao ndio wasimamizi wa mradi huo, wametangaza kuwa nauli hizo zitaanza kutumia rasmi Januari 16,2023 na kuweka bei za nauli hizo katika ruti tofauti.
“Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) unapenda kuwaarifu watumiaji wa mabasi yaendayo haraka kuwa kuanzia Jumatatu, Januari 16, 2023 nauli mpya zilizoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) zitaanza kutumika, ” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa nauli katika njia kuu ya Kimara-Kivukoni, Kimara-Gerezani na Kimara-Morocco itakuwa Sh750.
Kimara-Mbezi nauli itakuwa Sh500 wakati ile ya Kimara- Kibaha na Kimara-Mlongazila itakuwa Sh 700, Gerezani –Muhimbili itakuwa Sh750.
Kwa upande wa nauli mpya za taksi mtandaoni, Latra imeelekeza teksi zinazobeba abiria wanne nauli ni Sh3,000 hadi Sh4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kuna safari nyingine toka hapo nauli itaongezeka kwa Sh800 hadi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa Sh80 hadi Sh100 kwa dakika.
Wakati kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa Sh1,000 hadi Sh1,200 kwa kilomita moja na kikiibuka kikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh80 hadi Sh150 kwa dakika.
Pikipiki ya kubeba abiria wawili nauli elekezi itakuwa Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama safari itaongezeka kutoka nauli itaongezeka kwa Sh300 hadi Sh400 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh50 hadi Sh70 kwa dakika.
Nauli za pikipiki mtandao zinazobeba abiria wasiozidi watatu itakuwa Sh2,000 hadi Sh2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na safari ya ziada itakayongezeka nauli itaongezeka kwa Sh500 hadi Sh600 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo njiani kama foleni nauli itaongezeka kwa Sh70 hadi Sh90 kwa dakika moja.