Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nauli za SGR na ‘eti eti’ zake

Mabehewaaaaaaa Mapyaaaaa.jpeg Nauli za SGR na ‘eti eti’ zake

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likiwasilisha mapendekezo ya nauli za abiria kwa treni kwa njia ya Reli ya Kisasa (SGR) kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), wadau wa usafiri na maendeleo wamesema nauli hizo ni kubwa na TRC inapaswa kutoa huduma na si kufanya biashara.

Kulingana na mapendekezo ya nauli yaliyotolewa na TRC, nauli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro mtu mzima atapaswa kulipia Sh24,794 na Sh12,397 kwa mtoto kuanzia miaka (4-12) na kwa daraja la kati ni Sh29,752 na Sh14,876 kwa mtoto.

Kwa safari ya Dar es Salaam hadi Dodoma, TRC wamependekeza nauli ya Sh59,494 kwa mtu mzima na Sh29,747 kwa mtoto na kwa daraja la kati ni Sh71,392 na mtoto Sh35,696.

Hassan Mchanjama, mdau wa usafiri ardhini alisema TRC ni shirika la umma na miradi yote inayoendelea ni ya wananchi, hivyo huduma za usafiri wa reli hazipaswi kuchukuliwa kama sehemu ya biashara, bali utoaji wa huduma, kwani kufanya hivyo ni kuua mradi.

“Hali ya maisha kwa sasa ni ngumu, huduma ya vyakula imepanda, fikiria nauli zinapendekezwa hata nauli za basi ni ndogo, usafiri wa treni ndio wa bei ya chini duniani kuliko usafiri wowote.

“Miradi mikubwa inapotekelezwa ni ya wananchi, sioni sababu ya kuja kuwabebesha wananchi mzigo na hata ukiangalia hali ya maisha ni ngumu,” alisema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mdau wa maendeleo na mazingira, Dk Aidan Msafiri aliyesema kinachopaswa kuzingatiwa kwenye upangaji wa nauli ni haki na kupata faida ya kimaadili.

“Wazingatie wasipate hasara, lakini waangalie watu wanaopanda huku asilimia 92 ni watu wa chini, hawa wafikiriwe, hawataenda kupanda matajiri usafiri huo, wao wanapanda ndege, wazingatie Watanzania wengi wana kipato cha chini. Wawafikiriwe hawa,” alisema.

Dk Msafiri alisema katika upangaji huo wa nauli kuzingatiwe zaidi wadau watakaotumia usafiri huo. Joyce Mechack, mkazi wa Kihonda-Morogoro alisema kwa nauli zilizopendekezwa na TRC ni dhahiri mradi huo haujalenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini bali matajiri.

“Nawezaje kulipia Sh29,000 kwenye treni wakati nikipanda basi ni Sh10,000 na nikafika vizuri tu, kwa akili ya kawaida nawezaje kuchukua uamuzi wa kupoteza zaidi ya Sh19,000 kwa mara moja, nauli iwe chini ya usafiri wa basi, kila mtu kwenye maisha anatafuta unafuu,” alisema.

Mjadala huo umekuja kwa wengi wakilinganisha na nauli za mabasi, ambapo mchanganuo wa Latra unaonyesha nauli ya basi Dar- Moro kwa daraja la kati ni Sh11,000, wakati Dar -Dodoma ikiwa ni Sh26,000.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Domminick Lukiko alisema suala la upangaji wa nauli si la majadiliano, kwani hupangwa kulingana na uhalisia wa gharama zilizotumika.

“Labda Serikali iamue kuwabeba wananchi wake kwa kupunguza zaidi, lakini lengo la usafiri si starehe, ni kutoa huduma ya msingi kwa wananchi. Kwa uzoefu wa nchi nyingi huduma hiyo inakuwa ya kusaidia wananchi na si biashara, ili iwe biashara inapaswa iwepo na njia nyingine ili kama ni biashara mtu achague.

“Mfano kuna wazo la kuleta barabara ya kulipia, mtu ataweza kutumia barabara hiyo au atumie ya umma ambayo ipo, kwa hiyo cha kuzingatia wananchi wanataka huduma,” alisema.

Akizungumzia mapendekezo hayo ya TRC, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Leo Ngowi alisema wamepokea barua yenye mapendekezo ya nauli hizo na wataanza kufanyia kazi na kutoa mapendekezo yao hivi karibuni.

Alisema japo bado hawajafanyia uchambuzi mapendekezo ya TRC, yanayopaswa kuzingatiwa katika upangaji wa nauli ni kuangaliwa kwa huduma inayotolewa, upatikanaji wake kwa wakati na kwa viwango vinavyomridhisha mpokea huduma. Kwa upande wake, Msemaji wa Latra, Salum Pazzy alisema kwa sasa TRC wamewasilisha mapendekezo ya nauli hizo na wao kama Latra wameitisha maoni ya wadau na mamlaka hiyo ndiyo itakayotangaza nauli watakayoiona ni sahihi.

Kutokana na mapendekezo ya TRC, Latra imeitisha maoni ya wadau Desemba 19 mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa kifungu Na 21 cha Sheria Na 3 ya Latra ya mwaka 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live