Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nauli kutoka Moshi-Dar Sh10,000 tu

33081 MIOSHI+PIC Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Bei ya nauli kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro kwenda jijini Dar es Salaam imeshuka kutoka Sh32,800 hadi Sh10,000  

Hali hiyo inatokana na ongezeko la magari ya abiria yanayotoka jijini Dar es Salaam kwenda Moshi kukosa abiria pindi yanaporejea Dar es Salaam.

Hatua hiyo imejitokeza baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra) kuongeza idadi ya magari ili kuondoa adha ya usafiri kwa abiria wanaosafiri msimu huu wa Sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya.

Mmoja wa madereva wa magari yanayokwenda Dar es Salaam, Omari Hamza amesema kumekuwapo changamoto kubwa ya upatikanaji abiria wanaokwenda Dar es Salaam na baadhi ya magari kurudi bila abiria.

“Sasa hivi kwenye magari tunakosa abiria wanaokwenda Dar es Salaam, tunatafuta abiria kwa shida mno, imebidi angalau tushushe nauli lakini kitu ni kile kile.”

“Nahangaika hapa tangu asubuhi ili nipate angalau abiria wa kurudi nao lakini hakuna kabisa, cheki magari yalivyotupu hakuna waendaji,” amesema Hamza.

Naye mmoja wa viongozi wa kituo hicho cha mabasi, Aloyce Ndanu amesema magari mengi ya nyongeza yaliyoelekezwa na Sumatra kuleta abiria mkoani Kilimanjaro yamesababisha magari kuwa mengi hali ambayo imesababisha nauli kushuka.

“Sasa hivi magari hapa stendi yamekua mengi na abiria wanaosafiri kwenda Dar es Salaam hakuna, ni wachache mno, sasa tumeona kuliko magari yarudi bila abiria tushushe bei, haya ya nyongeza yaliyoletwa yanabeba abiria kwa Sh10,000 na magari makubwa hivyo hivyo kuanzia Sh10,000 hadi Sh15,000 kwa VIP,” amesema Ndanu.

Jane James ambaye ni miongoni mwa abiria anayesafiri kwenda jijini Dar es salaam amesema hiyo ni neema kubwa kwao na kusema ni jambo la kumshukuru Mungu.

“Sijawahi kusafiri nikatoa nauli ya Sh10,000 leo ni mara yangu  ya kwanza, pia nimeshangaa kuona magari yako matupu hakuna abiria kabisa, lakini changamoto ni kwamba tunakaa stendi muda mrefu mpaka abiria waongezeke kidogo ndio tuondoke,” amesema Jane.



Chanzo: mwananchi.co.tz