Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea fedha kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023 bungeni mjini Dodoma leo, Waziri Nape amesema watumiaji wa huduma hiyo wameongezeka kutoka 27,326,938 mwezi Aprili, 2021 hadi kufikia 35,749,298 mwezi Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 30.8.
“Watoa huduma wa Miundombinu ya Mawasiliano wamefikia 23 ukilinganisha na watoa huduma 19 Mwezi Aprili, 2021, hii ni sawa na ongezeko la asilimia 21.1.
“Bei ya mwingiliano kati ya watoa huduma (Voice interconnection Charges), imeshuka kutoka Sh 2.6 kwa dakika mwaka 2021 hadi Sh 2.0 kwa dakika mwaka 2022, sawa na punguzo la asilimia 23.1,” amesema.