Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu waziri ataka wakala wa maabara mifugo kujitathmini

10583 Pic+naibu TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameuagiza wakala wa maabara ya mifugo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Alitoa kauli hiyo juzi alipotembelea maonyesho ya wakulima (Nanenane) eneo la Nzuguni jijini Dodoma.

Ulega alisema hafurahishwi na utendaji wa wakala huo.

Akizungumza katika banda la wakala huo, Ulega alisema kitendo cha kuchelewesha majibu ya sampuli za magonjwa ya mifugo kinasababisha matatizo na hasara kubwa kwa wafugaji.

Naibu waziri huyo alisema kila wakati wafugaji wanalalamika kuwa majibu ya sampuli za magonjwa yamekuwa yakicheleweshwa hata kusababisha mifugo kufa.

“Hivi mnachukua muda mrefu kwa sababu gani, vipimo vyenu vinakaa muda mrefu na wafugaji wanalalamika huku mifugo ikiendelea kufa wakati mngekuwa na nafasi nzuri ya kuwasaidia kama majibu yangerudishwa mapema,” alisema Ulega.

Alisema kuna shida ya mifugo kutoroshwa na kupelekwa nchi jirani na kwamba, kwa mwaka zaidi ya mifugo milioni 1.5 hutoroshwa kwenda nje.

Pia, alizungumzia unywaji maziwa akisema wananchi wengi wako nyuma akisisitiza kampuni za usindikaji maziwa kubuni mipango ya kuwafikia waliko.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema wafugaji wa Kitanzania kwa sasa wanafuga kwa kukata tamaa kutokana na kushindwa kuihudumia mifugo ipasavyo.

Dk Mahenge alisema wataalamu wa mifugo wanatakiwa kuwa karibu na wafugaji ili kuwasaidia katika masuala ya kitaalamu.

Naye mwakilishi wa kampuni ya maziwa ya Asas, Lupyana Chengula alisema wameanza kusambaza bidhaa zao vijijini licha ya kukabiliwa na changamoto ya kutokuwapo umeme unaohitajika katika kutunza maziwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz